Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MOI yapokea wagonjwa 60 uvimbe ubongo

MOI MOI ina wataalamu 10 tu

Sat, 9 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), Imesema inapokea wagonjwa takribani 50 hadi 60 kwa mwaka wenye matatizo ya uvimbe kwenye ubongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respecius Boniface, alitoa takwimu hizo jana hospitalini hapo baada ya wataalam wa MOI kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka India, kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo bila kupasua fuvu la kichwa.

Dk. Boniface alitaja sababu za ugonjwa huo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza, watu wenye umri mkubwa na wengine kuzaliwa nao.

“Wagonjwa watatu hadi watano kila mwezi tunawapokea MOI, sijui hospitali nyingine na ambao hawafiki hospitali huko wapo wangapi,” alisema Boniface.

Pia alisema hadi sasa MOI imefanikiwa kufanya upasuaji wa kuondoa uvimbe bila kupasua fuvu la kichwa kwa wagonjwa 164 tangu kuanza kwa huduma hiyo Januari mwaka jana.

Alisema mafanikio hayo yametokana na serikali kuwekeza Sh. bilioni 7.9 kwa ajili ya kununua mashine ya kisasa ya matibabu, kujenga miundombinu na kuongeza ujuzi kwa wataalam.

“Wote mmeshuhudia mgonjwa anafanyiwa upasuaji, huku akiwa anaongea na kumaliza bila mgonjwa kupata shida yoyote,” alisema.

Dk. Boniphace alisema upasuaji huo unatumia njia ya mshipa wa fahamu uliopo kwenye paja kuelekea hadi kwenye ubongo kutoa matibabu hayo.

Alisema pia serikali iliingia ushirikiano na Hospitali ya India kwa ajili ya kuwafundisha watoa huduma za afya wa MOI wanaotoa huduma katika kitengo hicho.

Alisema madaktari hao wameendelea kuja nchini kutoa ujuzi kwa madaktari wazawa kuhusu matibabu hayo ili kuwajengea uwezo na baadaye watoe huduma hiyo wenyewe.

Dk. Boniface alisema tangu wataalam hao wamefika MOI siku tatu wamefanya upasuaji kwa wagonjwa watatu na mgonjwa mmoja anafanyiwa huduma ya upasuaji kwa dakika 30.

Alisema matibabu ya awali mgonjwa alikuwa akifanyiwa huduma ya upasuaji kwa muda wa wiki mbili, lakini kwa sasa mbinu hiyo mpya inatumia dakika 30.

Dk. Boniface alisema gharama za matibabu ya huduma ya upasuaji wa uvimbe kwenye kichwa nje ya nchi inategemea na hali ya mgonjwa lakini kwa wastani ni kati ya Sh. milioni 30 hadi 60, lakini kwa hapa nchini ni Sh. milioni tatu hadi sita.

Alisema pia wataalam wa ndani wataenda nje ya nchi kwenda kujifunza ujuzi wa aina hiyo ili kuongeza idadi kubwa ya wataalam.

Alisema mashine moja ya upasuaji inahitaji watalaam 10 hadi 15 wa kutoa matatibabu lakini sasa wapo 10, na kwamba kwa mwaka mashine hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 200 hadi 300.

Daktari Bingwa wa Mishipa ya Fahamu na Ubongo, kutoka kitengo cha Upasuaji wa Mishipa ya Ufahamu na Ubongo MOI, Dk. John Mtei, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kutoa matibabu mapema kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo na kupunguza foleni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live