Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MOI yapandikiza nyonga bandia kwa njia ya kisasa

41904 Pic+moi MOI yapandikiza nyonga bandia kwa njia ya kisasa

Sat, 16 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na hospitali ya Zydus ya nchini India imefanikiwa kupandikiza nyonga bandia na upasuaji wa mgongo kwa njia ya kisasa.

Madaktari walitumia saa moja kumfanyia upasuaji wa mgongo mgonjwa, operesheni ambayo ingehitaji takriban saa tatu kwa njia za kawaida. Madaktari pia walitumia saa mbili kupandikiza nyonga badala ya tano zilizokuwa zikitumika awali.

Upasuaji huo umepangwa kufanyika kwa wagonjwa wengine zaidi ya sita, kati ya jana na Februari 16.

Akizungumza mara baada ya operesheni hiyo, mkurugenzi mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya MOI na Zydus.

“Awali, tulishirikiana katika kliniki maalumu na safari hii wamekuja kwenye kambi hii ya upasuaji. Naamini madaktari wetu watapata mbinu mpya na za kisasa ili waendelee kutoa huduma hizo hata baada ya wageni hawa kuondoka,” alisema Dk Boniface.

Taasisi hizo mbili zilisaini mkataba wa ushirikiano mwaka 2018, ambao unalenga kubadilishana uzoefu, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kubadilishana teknolojia, uboreshaji wa miundombinu pamoja na utafiti.

Mkuu wa kitengo cha uhusiano wa kimataifa wa Zydus, Himsnshu Sharma alisema ushirikiano huo umekuwa na mafanikio na unanufaisha wagonjwa kwa kuwapa huduma kwa kutumia mbinu za kisasa bila ya kusafiri kwenda nje ya nchi.

“Teknolojia na mbinu za upasuaji zinabadilika kila siku na kwa kuwa tunashirikiana, wataalamu wetu wameleta mbinu mpya ambazo tunazitumia kule India,” alisema Sharma.

Daktari bingwa wa mifupa wa MOI ambaye amejikita katika upandikizaji wa nyonga bandia, Dk Violeth Lupondo alisema mbinu wanazopata zitawasadia kuendelea kutoa huduma hizo hata baada ya madaktari kutoka Zydus kuondoka.



Chanzo: mwananchi.co.tz