Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MOI yaleta matumaini wanaopatwa kiharusi

MOI Hospitali ya Muhimbili

Tue, 6 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

Akizunguma katika banda la taasisi hiyo kwenye Maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), Muuguzi katika chumba cha upasuaji kutoka taasisi hiyo, Juma Rehani, alisema ndani ya saa hizo sita hadi 12 mgonjwa wa aina hiyo akiwahishwa kufanyiwa uchunguzi na kutibiwa katika taasisi hiyo anaweza kupata nafuu na kurudi katika hali yake ya kawaida.

“Na siyo tu kwenye ubongo, pia kwenye uti wa mgongo na sehemu mbalimbali za mwili. Wagonjwa waliopata kiharusi, ndani ya saa sita mpaka 12 wakifika kwenye huduma hii anaweza akapata nafuu na akarudi kwenye hali yake ya kawaida,” alisema Rehani.

Alisema huduma hiyo ya tiba ni mpya na imeanza  tangu Januari mwaka huu na hutolewa bila kupasua kwenye eneo la mwili ambalo linakuwa limeganda damu badala yake hutumia tundu dogo kupitia sehemu ya nyonga kuingiza mpira.

Alisema huduma hiyo inahusika zaidi na wagonjwa ambao wamepata matatizo ya kwenye mishipa ya damu iliyopo kwenye ubongo.

“Katika ubongo kuna mzunguko wa mishipa ya damu ambayo ikitokea ikipata hitilafu na damu ikaganda, na inapoganda kwa kutumia upasuaji wa kawaida, huwezi kutoa tone la damu lililoganda, kwa hiyo njia ya kisasa ambayo inatumika ni kutumia mipira kupitia kwenye nyonga kupitia mshipa mkubwa ambao unapeleka mpaka kwenye ubongo,” alisema Rehani.

“Kuna wale wagonjwa ambao wanakuwa wamepata kitu  kinaitwa  kiharusi ambao damu imevujilia kwenye ubongo ambao katika kupitia mashine ya kisasa ambayo kwa Afrika Mashariki na Afrika ya Kati inapatikana MOI peke yake, ina uwezo mkubwa sana wa kufanya uchunguzi pamoja na matibabu kwenye mishipa ya damu.”

Alisema tangu huduma hiyo ianze, tayari wameshawahudumia wagonjwa 27, na kwamba bado wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili wale waliokuwa wakipewa rufani kwenda kutibiwa hospitali nje ya nchi watibiwe katika taasisi hiyo.

“Na tunaendelea na taratibu za kutoa matibabu, kufanya uchunguzi, hivyo mtu akipata matatizo akifika MOI atakutana na madaktari bingwa watamwangalia na baada ya hapo watampeleka kwenye uchunguzi kujua tatizo la mshipa wa damu limetokea sehemu gani ya ubongo au sehemu gani ya uti wa mgongo,” alisema Rehani.

“Lakini kuna wale ambao wanakuwa wamepata uvimbe kwenye ubongo na wanahitajika kwenda kufanyiwa upasuaji wa kufungua fuvu, kwa kutumia mashine hii ina uwezo wa kutumia mpira kwenye kitundu kidogo na kwenda kufunga ile mishipa ya damu ambayo inaenda kwenye ule uvimbe ili kupunguza uwezekano wa mgonjwa wakati wa kufanyiwa upasuaji asivuje damu kwa wingi.”

“Kwa hiyo tunapofunga mishipa ya damu inarahisisha upasuaji kwa njia ya usalama zaidi.”

Alisema kabla ya taasisi hiyo kuanzisha huduma hiyo, Januari mwaka huu gharama za uchunguzi na matibabu ambazo watu walikuwa wakizitumia kwenda nje ya nchi kutibiwa zilikwa kubwa zaidi.

“Ukienda nje ya nchi kutibiwa ugonjwa huu, gharama za uchunguzi pekee  ni Sh. milioni 10 hadi 15 na matibabu yake ni zaidi ya Sh. milioni 20,” alisema Rehani.

“Gharama za uchunguzi kwa taasisi yetu ni kuanzia Sh. milioni 2.5 hadi 4.5 kwenye hatua ya uchunguzi. Kwenye hatua ya tiba bado tunaendelea na uchunguzi kwenye kitengo hiki ili tujue gharama halisi ya matibabu.”

Chanzo: ippmedia.com