Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MOI yachunguza mishipa kwenye ubongo bila upasuaji

9a87f607dc65ca16e90240c770fd76dd MOI yachunguza mishipa kwenye ubongo bila upasuaji

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Mifupa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) kwa mara ya kwanza imetoa huduma ya uchunguzi wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu la kichwa.

Uchunguzi huo umefanywa kwa saa tatu katika maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo na jopo la madaktari bingwa, wauguzi, watalamu wa radiolojia wazalendo sita kutoka MOI, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Hospitali ya Agakhan.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface amesema kuanza kwa maabara hiyo ni ishara ya mageuzi makubwa katika sekta ya afya hapa nchini kwani maabara kama hiyo haipo kwenye nchi nyingine kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Leo (jana) ni siku ya furaha sana kwani tumeanza kutumia maabara yetu ya upasuaji wa ubongo, hii imewezekana kutokana na dhamira ya dhati ya Rais John Magufuli kuboresha huduma za afya nchini kwani maabara hii imejengwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa zaidi ya Sh bilioni 7.9,” alisema Dk Boniface.

Naye Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo MOI, Dk Lemery Mchome alisema kuanza kwa maabara hiyo kumeleta mageuzi makubwa katika huduma za uchunguzi na upasuaji wa ubongo nchini, kwani hakuna mgonjwa atakayelazimika kwenda nje ya nchi kufuata huduma hiyo ambayo ilikuwa haipatikani nchini.

“Tunashukuru upasuaji umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa, tumeweza kufika kwenye ubongo wa mgonjwa bila kufungua fuvu, tumefanya upasuaji huu katika mazingizra mazuri kwani mitambo hii ni ya kisasa sana, mgonjwa yuko macho na anaongea vizuri, hana kovu wala maumivu, hii ni hatua kubwa sana kwetu kama wataalamu,” alisema.

Kwa upande wake, mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huo, Hafidhi Saidi kutoka mkoani Singida amemshukuru Mungu kwa huduma aliyopata kwani alikuwa akipata maumivu kwa kipindi kirefu bila kujua anasumbuliwa na ugonjwa gani.

“Pia namshukuru sana Rais John Magufuli kwa kununua vifaa hivi ambavyo vimesaidia kuhudumiwa hapa MOI, nawashukuru madaktari na wataalamu wote walionihudumia, nimefurahi sana na nawaambia Watanzania wenzangu wenye shida kama yangu waje wahudumiwe hapa MOI,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz