Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), imeanzisha huduma mpya ya utengenezaji wa mkono wa umeme ambapo hadi sasa tayari wagonjwa watano wamehudumiwa.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Abel Makubi, wakati akielezea utekezaji wa majukumu na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Amesema wagonjwa watano wameshahudumiwa, gharama zake ndani ya nchi ni Sh15 milioni na nje ya nchi ni Sh30 milioni hadi Sh60 milioni. Profesa Makubi amesema mkono huo unaweza kufanya baadhi ya shughuli ambazo mtu angeshindwa kuzifanya akiwa hana mkono huo.
“Anaweza kujisaidia hata kula na kufanya vitu vingine au kutembea kwa kutumia mfumo ambao umeprogramiwa kwa kutumia umeme. Kwa wananchi ambao tumewawekea umeweza kuwasaidia kwa baadhi ya vitu ambavyo walitegemea kuwa kwa asilimia 100 wasingeweza kuzifanya,”amesema.
Amesema kuwa mkono huo umewawezesha kufanya kazi asilimia 60 hadi 70 ambazo walikuwa wameshindwa kuzifanya.