Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MNH waongeza huduma mpya za lishe Sabasaba

D02e70eb24186701f421e082f09fa963.jpeg MNH waongeza huduma mpya za lishe Sabasaba

Fri, 2 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imeongeza huduma mpya ya lishe na ushauri kuhusu mtindo bora wa maisha, ngozi na meno kwa ajili ya wananchi wanaotembelea Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu, Sabasaba.

Akizungumza na HabariLEO katika maonesho hayo, Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Neema Mwangomo, alisema wameamua kuongeza huduma hizo zinazotolewa bila malipo ili kuwasaidia watu kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

“Tumeona tuongeze hizi huduma kuwafikia watu wengi zaidi hapa, mteja akipimwa akionekana ana tatizo linalohitaji uchunguzi zaidi, atapewa rufaa ya kwenda katika Hospitali ya Muhimbili ya Upanga au Mloganzila.

“Ushauri hapa na huduma za tiba unatolewa bila malipo, hivyo watu waje kwa wingi kujua afya zao. Mtindo wa maisha tunaoishi unatugharimu zaidi na tunaugua kimya kimya, hivyo kujua kama una tatizo mapema inasaidia kuondoa madhara makubwa zaidi,” alisema Mwangomo.

Akizungumzia huduma za lishe, Mtaalamu wa Lishe wa MNH, Scholastica Mlinda, alisema wanawapokea wateja na kuwapima vitu muhimu kwanza ikiwamo shinikizo la damu na kufanya nao mazungumzo kujua mtindo wa maisha walio nao na namna ya ulaji wa mtu kisha kumshauri.

“Tukishamfanyia vipimo vya awali, tunamshauri apunguze nini na nini aongeze. Lakini katika ulaji, mtindo wetu wa maisha wa kula wanga zaidi kuliko matunda na mboga ndio unasababisha magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza na hivyo kupunguza nguvu kazi ya taifa,” alisema Mlinda.

Alisisitiza jamii kuzingatia kula zaidi matunda na mboga zenye rangi zote kwa kuwa kila rangi ina maana yake mwilini.

Mengine muhimu ni kupata muda wa kutosha wa kupumzika na ikiwa mtu atakutwa na uzito mkubwa kuliko unaopaswa, anaelekezwa namna ya kupungua kwa afya.

Mwangomo alisema mbali na huduma hizo mpya, pia wanaendelea na huduma zote ikiwamo za dharura na gari la wagonjwa lipo tayari kwa watakaopewa rufaa, huduma za macho, meno na zinatolewa na madaktari bingwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz