Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MATIBABU: Hospitali Mloganzila lawamani kwa madai ya huduma hafifu

91042 Pic+mloganzila MATIBABU: Hospitali Mloganzila lawamani kwa madai ya huduma hafifu

Tue, 7 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila iliyopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam imeingia katika lawama za utoaji huduma hafifu, kutoza gharama kubwa na kukosekana kwa maeneo ya kusubiria wagonjwa waliolazwa.

Hospitali hiyo iliyozinduliwa Januari, 2017 pia imelalamikiwa kwa ucheleweshwaji wa huduma na kutopatikana kwa taarifa za wagonjwa.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Wazee na Watoto imekiri kupata malalamiko ya wananchi hasa katika mitandao ya kijamii na kuahidi kutoa taarifa rasmi.

Kiini cha tatizo

Baadhi ya ndugu wa wagonjwa waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walilalamikia wafanyakazi wa kitengo cha radiolojia wakisema wamekuwa wakichelewesha majibu ya vipimo vyao kiasi cha kupata madhara ya kupoteza viungo na wengine kufariki dunia.

Aluu Segamba, aliyepoteza ndugu yake wiki moja iliyopita ni miongoni mwa watu waliozungumza na Mwananchi kulalamikia matatizo ya hospitali ya Mloganzila.

“Mgonjwa wangu alifariki pale Mloganzila. Alilazwa Hospitali ya Amana na tulipewa rufaa ili akafanyiwe kipimo cha CT Scan ya kifua na siku ileile tumefika alipimwa.

“Tatizo lilikuja kwa wataalamu wa CT Scan, mgonjwa wangu alikaa siku tano bila kupatiwa majibu, hadi anaaga dunia alikuwa hajaanzishiwa matibabu ya tatizo lake wakati madaktari wa wodini walikuwa wamejipanga kumtibu,” alieleza Segamba.

Mgonjwa mmoja, ambaye hakutaka jina lake litajwe alidai ilimchukua siku 21 kupata majibu ya vipimo vyake na kusababisha mguu wake kukatwa.

“Wagonjwa wengi wanapoteza maisha hapa kwa sababu ya kukosa huduma, wodi niliyolazwa haikuwa ya mifupa, lakini vipimo baadaye vilionyesha nilikuwa na shida hiyo hadi napelekwa kwenye upasuaji mguu ulishaoza nikakatwa,” alieleza mgonjwa huyo.

Kuhusu upungufu wa wataalamu, Ally Yusuph, ambaye ni mmoja wa ndugu wa wagonjwa alisema ilimchukua siku mbili kumwona daktari tangu alipofika hospitalini hapo Desemba 16, 2019.

Atuganile Mboya anayeuguza dada yake anasema hofu kubwa kwake ni kupoteza ndugu yake kutokana na taarifa zilizopo.

“Kila ninayemwambia tumelazwa Mloganzila ananiambia hapo hakuna huduma nzuri, hili suala limekuwa likinichanganya sana,” alieleza Mboya.

Gharama za huduma

Akizungumzia gharama kuwa juu, mgonjwa mmoja alisimulia kuwa alilazwa hospitalini kwa wiki mbili hapo akipokea matibabu, kabla ya kupelekewa bili ya zaidi ya Sh2 milioni gharama ambazo asingeweza kuzilipia, hivyo aliacha vitu vyote na kuondoka.

“Niliona hata nikiuza mali nilizonazo, siwezi kulipa na ndugu zangu walikata mguu kunitembelea kwa kuwa waliona wasingelimudu. “Nimepanga nyumba hapa Dar es Salaam, kazi yangu nauza mbogamboga na nina watoto wawili wananitegemea. Sikupenda kufanya uamuzi huo lakini nilipelekwa kwa rufaa, nashukuru nilipata huduma nzuri hadi kupona ila tatizo likawa gharama za matibabu ambazo zilikuwa kubwa,” aliongeza.

Miundombinu wezeshi

Wakati hospitali hiyo ikiwa inatoa huduma ya chakula cha mchana kwa wagonjwa wote, bado ndugu wanahitajika kufika asubuhi kabla ya saa moja asubuhi na saa 10.00 jioni kwa ajili ya kusaidia wagonjwa waliolazwa.

Jane Japhet kutoka Turiani mkoani Morogoro anasema hali kwake ni mbaya kwani yeye na mwanaye wanalazimika kulala na kushinda nje ya hospitali ili kumwangalia mama yake aliyelazwa hospitalini hapo.

“Muhimbili kuna eneo maalumu limetengwa kwa ajili ya wanaouguza wasio na makazi hapa Dar es Salaam, tunalala huko. Hapa Mloganzila hali ni tofauti hakuna eneo lililotengwa na kwa bahati mbaya nimekuja na mtoto huyu mdogo,” anaongeza Jane.

Naye Othman Sanga aliyetokea Makete mkoani Njombe alieleza kushangazwa na hospitali hiyo kutokuwa na eneo kwa ajili ya watu wanaoangalia jamaa zao waliolazwa.”

Kauli ya Serikali

Akizungumzia malalamiko hayo, naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Faustin Ndugulile alisema wizara hiyo ina taarifa za matatizo ya hospitali hiyo na inazifanyia kazi.

“Ninachoweza kusema tutatoa taarifa kama wizara hususani watu wanaosema wanakatwa miguu, tutasema kwa sababu tunazo takwimu zote. Tunafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora,” alisema.

Akizungumzia eneo la watu wanaowahudumia wagonjwa wao, Dk Ndugulile alisema; “Kiutalaamu mgonjwa hapaswi kulala na ndugu kwa sababu ni hospitali ndiyo inayomhudumia mgonjwa. Lakini kumekuwa na utamaduni wa watu kutaka kulala na wagonjwa wao.”

Dk Ndugulile alisema pia watu wengine ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam hukaa hospitalini hapo kwa kuhofia kutumia nauli ya kurudi mchana kuwaona wagonjwa wao.

ili kuokoa nauli ya kwenda na kurudi.

“Mtu akienda Mloganzila asubuhi na kutakiwa kurudi mchana, basi anaona bora akae palepale ili kupunguza gharama. Tumejaribu kuboresha mazingira ya watu kusubiria lakini haturuhusu mtu kulala na mgonjwa ili kuepusha hatari ya kuambukizana magonjwa,” aliongeza Dk Ndugulile.

Kuhusu madai ya gharama ya huduma za hospitali hiyo, alisema zinaendana na aina ya huduma anayopata mgonjwa.

“Gharama zinapungua kwa mambo mawili, bima ya afya na pili zinapungua endapo mgonjwa atafuata mfumo wa rufaa. Kama ataanzia kituo cha afya akaenda hospitali ya wilaya, akashindwa akaenda hospitali ya mkoa na kuletwa Mloganzila, gharama yake inakuwa nafuu sana tofauti na mtu aliyepelekwa moja kwa moja,” aliongeza Ndugulile

Chanzo: mwananchi.co.tz