Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAT yataka hatua kuzuia wimbi la tatu la corona

40522a1ced25ce78a984749432883311.jpeg MAT yataka hatua kuzuia wimbi la tatu la corona

Tue, 22 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeanisha hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepusha wimbi la tatu la kuingia na kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.

MAT kimeanisha hayo zikiwa ni siku chache baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoa hadhari juu ya tishio la mlipuko wa wimbi la tatu la maambukizi ya Covid-19 nchini.

Akizungumza na HabariLEO Dar es Salaam jana, Rais wa MAT Dk Shedrack Mwaibambe, alitaja baadhi ya hatua zinazopaswa kufanywa kuwa ni pamoja na kudhibiti idadi ya abiria katika vyombo vya usafiri na kuweka idadi ndogo ya mikusanyiko ya watu katika matukio.

“Ni vyema serikali ikiwa na uwazi zaidi katika kuwasaidia wananchi na si tu kusema kuwa kuna viashiria na kwa sababu kamati iliundwa, nashauri watangaze kama ugonjwa upo au haupo ili kila kitu kiwe wazi,” alisema.

Akaongeza: “Kama ugonjwa upo, basi tahadhari zichukuliwe kwa kuunda sera au sheria ndogo kama vile kupunguza idadi ya watu katika vyombo vya usafiri kwani bado msongamono upo katika vyombo hivyo, kuweka idadi ya watu katika matukio kama vile harusi na matukio mengine yenye mikusanyiko na pia, kuzingatia matokeo yaliyotolewa na kamati ile iliyoundwa na Rais.”

Uchunguzi wa HabariLEO katika maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam umebaini kuwa, licha ya hadhari hiyo, hakuna tahadhari zinazochukuwa kuepusha maambuzi isipokuwa katika baadhi ya ofisi na mikutano mikubwa ya kiserikali.

Mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Karume jijini Dar es Salaam, Sheila Juma, alisema watu wengi wamejisahau na kuchukulia suala la corona kama jambo la kawaida.

“Kwa kweli hakuna tahadhari zozote zinazochukuliwa na watu maana kama ni kwenye daladala, bado tunabanana na hata hapa sokoni bado watu ni wengi, msongamano ni mkubwa na watu hawavai barakoa,” alisema.

Akaongeza: “Nashauri serikali iongeze juhudu za kutoa elimu zaidi kwa jamii kuhusu umuhimu wa kila mtu kujikinga awe na mwitikio wa hilo.”

Kwa mujibu wa MAT, wananchi wanapaswa kuwa makini kwa kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono.

Chanzo: www.habarileo.co.tz