BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema imeridhishwa na ukaguzi wa abiria wanaotoka nje ya nchi wanaotumia Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3).
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt Masatu Chiguma amesema hayo leo baada ya kumalizika kwa ziara yao ya kwanza ya kikazi tangu kuteuliwa kwao hivi karibuni ambapo wametembelea jengo hilo kuwa maafisa afya waliopo kwenye Jengo hilo wanafanya ukaguzi kulingana na taratibu zilizowekwa, ili kuzuia maambukizi ya Homa Kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi aina ya Corona, isiingie nchini. Dkt Chiguma amesema tahadhari ya kuzuia ugonjwa huo ulioanzia nchini China na kusambaa kwenye nchi mbalimbali Duniani, imefanyika ipasavyo kwenye Jengo hilo, baada ya kulitembelea na kuona, vifaa na utendaji wa watumishi hao wa afya.
“Matayarisho ya kujihadhari na huu ugonjwa wa Corona yamefanyika kwa hali ya juu na wajumbe wa Bodi tumeridhika baada ya kuona vifaa vinavyohitajika kuvaliwa na watendaji wa kitengo cha afya na pia watumishi wa TAA waliopo maeneo ya kuwasili na maeneo mengine,” amesema.
Akizungumzia jengo hilo, Dkt Chiguma amesema anaipongeza serikali kwa ujenzi wa jengo hili la kisasa lenye vifaa vya kimataifa, ambapo uendeshaji wake ni wa hali ya juu. “Tumepita kuanzia mwanzo wa jengo hadi mwisho wa jengo na tumejionea namna lilivyo bora na zuri, hata vifaa vyake ni vya kitaalam sana, ukiangalia eneo la mizigo ni mashine tu zinafanyakazi pamoja na kuwa na Watumishi wachache lakini kila kitu kinaongozwa na mashine za kisasa,” amesema. Hatahivyo, amesema Bodi imebaini bado katika jengo hili kuna upungufu mkubwa wa watumishi, ambapo sasa waliopo wengi ni wanaofanya kazi kwa mikataba mifupi na wale wanaendelea kujifunza (Internship), ambapo ni hatari kwa kuwa sio wakutegemewa zaidi kutokana kuweza kuondoka wakati wowote watakapopata ajira ya kudumu. Pia ameitaka menejimenti ya TAA kuhakikisha inaboresha maslahi ya watumishi ili waendelee kulitunza jengo hilo kwa kufanya kazi kwa bidii.