Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lupaso walilia mawasiliano, maji, chumba cha upasuaji

E03e583e901c062910396e690ee16752 Lupaso walilia mawasiliano, maji, chumba cha upasuaji

Wed, 29 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANAKIJIJI cha Lupaso ikiwemo familia ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, wameiomba serikali isiwasahau katika kufanyia kazi changamoto alizotamani kuzimaliza wakati wa uhai wake zikiwamo za maji, mawasiliano na ujenzi wa chumba cha upasuaji katika zahanati ya kijiji hicho.

Rafiki wa karibu wa Mzee Mkapa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Masoud Rajabu aliiomba serikali iwaangalie watu wa Lupaso waliobaki kwa kuhakikisha zahanati ya kijiji iliyopewa hadhi ya kituo cha afya, iletewe madaktari wa kutosha ili wanakijiji wasiteseke ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Mkapa.

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupaso wakati Mkapa akiwa rais, Athanas Luchapa, alisema Mkapa alipokuwa madarakani alifanya mengi ya kitaifa na kwa kijiji hicho pia, alishiriki kukarabati kituo cha afya cha kijiji hicho na alisisitiza akipata changamoto ya afya akiwa kijijini, huduma ya kwanza ataipata Lupaso.

“Tulikuwa tukizungumza mara kwa mara akiniambia hatatibiwa Ndanda (Hospitali ya Misheni) bali hapa hapa kijijini, hivyo alikiangalia kituo hiki cha afya kwa jicho la tofauti sana. Aliyoahidi sijui sasa atafanya nani,”alisema Luchapa.

Aliiomba serikali isiwasahau watu wa Lupaso kwa sababu Mkapa amefariki dunia, bali imuenzi kwa kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo ujenzi wa chumba cha upasuaji na kero ya maji ambayo Mkapa alijitahidi kuipunguza.

Kwa upande wake, mtoto wa dada yake Mkapa, Dk Joseph Mkapa, aliiomba serikali iwakumbuke wanakijiji wa Lupaso katika kutatua changamoto kuu mbili alizosema hata mjomba wake (Rais mstaafu Mkapa) zilimkera na alijitahidi kuzipatia ufumbuzi bila mafanikio.

“Naiomba serikali itusaidie katika mambo makuu mawili; kwanza ni suala la mawasiliano, hili lilimkera Rais Mkapa hata wakati mwingine alikuwa hatamani kukaa hapa maana anakosa mawasiliano nanyi mnafahamu alikuwa mtu wa habari,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba kampuni ya simu ya Airtel ilifunga mnara kijijini hapo miaka ya nyuma, lakini mtandao umekuwa wa taratibu usio na nguvu, jambo ambalo ni kero kubwa kwa wakazi wa hapo katika mawasiliano.

Alisema eneo jingine ni Kituo cha Afya cha Lupaso kilichozinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Aliiomba serikali ikarabati hospitali hiyo hasa kusaidia kujenga chumba cha upasuaji, jambo alilotamani kulifanya mzee Mkapa.

Chanzo: habarileo.co.tz