Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lissu kuishi na risasi kwenye uti wa mgongo

14681 LISSU+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu hatafanyiwa upasuaji mwingine, lakini ataendelea kubaki na risasi moja kwenye uti wa mgongo.

Hayo yalielezwa jana kaka yake, Wakili Alute Mugwahi alipozungumza na wanahabari.

Alisema Lissu hatafanyiwa upasuaji mwingine baada ya kufanyiwa zaidi ya mara nne akiwa Ubelgiji ingawa kuna risasi moja ambayo imebaki nyuma ya uti wa mgongo.

“Wakijaribu kuitoa huenda ikaathiri uti wa mgogo na hivyo kupata tatizo la kupooza,” alisema.

Alisema risasi hiyo imeachwa kwa sababu haina athari kwa maisha yake.

“Si mara ya kwanza kwa mgonjwa kubaki na risasi mwilini kwani haitasababisha madhara makubwa, lakini ikitolewa huenda ikasababisha madhara,” alisema.

Lissu alihamishiwa hospitali ya Leuven iliyopo Ubelgiji akitokea Hospitali ya Taifa ya Nairobi, baada ya kushambuliwa kwa risasi kadhaa na watu wasiojulikana Septemba 7 mwaka jana akiwa Dodoma.

Alute, ambaye amerejea nchini wiki hii akitokea Ubelgiji kumjulia hali Lissu, alisema huenda mwanasiasa huyo akarejea nchini mwakani kwani mfupa wa mguu wake mmoja haujaunga vizuri na hivyo anahitaji uangalizi wa mara kwa mara.

Wakili Alute alisema bado Lissu hajapata ruhusa ya moja kwa moja kutoka kwa daktari wake hivyo atakuwa akipata huduma katika nyumba anayoishi karibu na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Ubelgiji.

“Haiwezekani kurudi karibuni, mimi nadhani labda mwakani hasa kutokana na kuhitaji uangalizi wa daktari wake, ingawa yeye na hata sisi wanafamilia tungependa arudi mapema,” alisema.

Alute aliwashukuru Watanzania wote wakiwamo wanaoishi Ubelgiji kutokana na michango wanayotoa kumsaidia Lissu na kwenda kumjulia hali.

Akizungumzia upelelezi wa tukio la kushambuliwa, alisema hadi sasa miezi takriban 11 imefika tangu tukio hilo lakini Lissu hajahojiwa wala dereva wake ambaye naye bado yupo Ubelgiji.

“Lissu anasikitika sana kwani hakuna upelelezi wa tukio lake ingawa ni Mtanzania na ana haki ya tukio lake kufanyiwa upelelezi ili wahusika wakamatwe,” alisema.

Alisema bado familia inamuomba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili waletwe wapelelezi kutoka nje ya nchi kushirikiana na wapelelezi wa ndani kubaini waliohusika na tukio hilo. Serikali imekuwa ikisema kuwa ina uwezo wa kupeleleza suala hilo yenyewe.

limewaandikia barua kuwa halitagharamia kwa kile kilichodaiwa kuwa, Lissu aliondoka nchini kutibiwa bila kufuata utaratibu wa bunge.

“Hivi sasa tunahangaika Lissu apone hili suala la matibabu kugharamiwa na bunge tutalishughulikia baadaye,”alisema.

Daktari wa Wizara ya Afya, Angel Ramadhani alisema risasi inaweza isilete madhara au ikaleta kulingana na sehemu ilipokaa.

“Inategemea imekaa sehemu gani, lakini mara nyingi daktari anayemshughulikia mgonjwa hujua iwapo risasi hiyo ikikaa inaleta madhara au la,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz