Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Laana nne kwa mwanamke anayetoa mimba

D58260d4c7af1572815b1464735f1d0e Laana nne kwa mwanamke anayetoa mimba

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KITABU: “Mama! Why Did You kill Us?” kilichoandikwa na Domenico Mondrone na kupigwa chapa na Tan Books and Publishers, Inc. Rockford, Illinois kinasimulia kisa cha mwanamama aliyetoa mimba saba na yaliyomfika baadaye.

Kinasema akiwa sasa anashambuliwa na kwikwi, wasiwasi, kilio, huzuni na kujikatalia, kukosa amani na utulivu na hali ya hofu na maumivu mara kwa mara, usiku mmoja akiwa amelala, alisikia sauti ya mtoto mchanga ikiita: “Mamaaa!” Hakujua sauti ilitoka wapi. Baada ya robo saa alisikia sauti za watoto wengi zikiita: “Mamaaa! Mamaaa!” Kisha ziliita tena: “Mamaaa!” tena kwa karibu zaidi.

Akajiuliza: “Je, haya ni mashetani?” Alifikiri labda alikuwa anaanza kupata dalili za wendawazimu. Akajikakamua akauliza: “Lakini ni nani anayeniita?” Wale watoto wakamjibu: “Ni sisi mama”.

Akauliza tena: “Ninyi ni nani?” Wakamjibu: “Ni sisi watoto wako ambao hukuturuhusu tuzaliwe.” Mama huyu akaishiwa nguvu. Akawasikia tena wakimwambia: “Tazama wote saba tuko hapa pamoja nawe.”

Baada ya pale aliona vivuli vya watoto saba vikitembea kati yake na ukuta na vikiwa vinabadilishabadilisha umbile. Akajiuliza: “Je, nimekuwa kichaa?” Wale watoto wakamjibu: “Hapana, wewe si kichaa, unachokiona ni ukweli mtupu. Unajisikia tu mkosaji baada ya kutuua tukiwa tumboni mwako. Sisi siyo vivuli, bali watoto halisi.”

Sauti ikaendelea: “Kama unataka ukweli, tutakudhihirishia jambo hilo. Saa chache ziliyopita, baba yetu amekufa, lakini hayuko nasi.” Yule mama alizimia kwa jinsi wale watoto walivyomwangalia kisha wakatoweka.

Naye Don Baker katika kijitabu “Beyond Choice” kilichochapishwa na Multnomah Press, Portland, Oregon, 1985 anasimulia masaibu yaliyomkumba mwanadada Debbie. Debbie alipata ujauzito ambao haukuwa na matarajio baada ya tendo moja tu la ngono akiwa sekondari.

Baada ya ujauzito huo, alijisikia mnyonge; alikuwa hatoki nje ya chumba chake na hata chakula alikuwa akipelekewa huko. Siku moja mama yake alimchukua na kumpeleka katika kituo cha kutolea mimba na kulipia Dola za Marekani 225.

Baada ya kutoa mimba hiyo Debbie na Tim, mshikaji wake walitoroka nyumbani na kwenda kujitegemea. Wakiwa huko Debbie alianza kutumia huduma za uzazi wa mpango, lakini hata hivyo alipata mimba tena na kuitoa baada ya kugundua ‘mshikaji’ wake alimtelekeza, hakuwa na fedha za kujihudumia na kumhudumia mtoto, na umri wake ulikuwa mdogo.

Alirudi kwa wazazi wake na kurudi shuleni kumaliza masomo yake, lakini tayari alikuwa ‘amepondeka na kujeruhiwa.’ Baada ya hapo, Debbie alibadilisha wavulana akapata mimba baada ya nyingine na zote alizitoa. Kutokana na kufukuzwa na wanaume aliokuwa nao kimapenzi na waliompatia mimba na hata msongo wa mawazo , alifukuzwa kazi.

Alijisikia mpweke, baada ya kukosa mtu wa kumfariji. Akatumia muda mwingi kulia. Alipotakiwa na mshauri nasaha kueleza jinsi anavyojisikia, Debbie akasema anajiona ametenda dhambi ya kuua, anajisikia kutengwa, anaijiona mwenye hasira na maumivu makali, anajisikia mkosaj na kwamba, anajiona mtu asiyekuwa na lengo la maisha.

Maisha ya Debbie yalirudi katika hali ya kawaida baada ya kupokea ushauri nasaha na uponyaji. Katika uponyaji Debbie alitakiwa kukiri na kutamka waziwazi kuomba msamaha kwa Mungu.

Baada ya sala hiyo, Debbie alilia kimyakimya; akaanza kujisikia mwenye amani na shukrani kuu. Usiku alipata usingizi mzuri wenye amani. Debbie alipata mchumba Steve na wakafunga ndoa na kuishi maisha ya amani. Kimsingi, laana kama kisababishi cha madhara au maumivu au huzuni au mateso, katika utoaji mimba inatokana na ukiukaji wa Amri za Mungu.

Uuaji ni kosa linalokwenda kinyume na matashi ya binadamu ya kuheshimu na kulinda uhai wa binadamu. Biblia Takatifu (Kut. 20:13) inasema: “Usiue.” Hii ni Amri ya Sita ya Mungu.

Ifahamike kuwa, wataalamu wa saikolojia wamefanya majumuisho kwa kuangalia laana za kisaikolojia wanazopata wanawake baada ya kuwaua watoto wao kabla ya kuzaliwa kuwa ni pamoja na kujihisi mkosaji na mwuaji, kujihisi umepotelewa na kitu fulani maishani, kulia na kujutia, kuhangaika na kukosa amani, kuweweseka na maono, upoteza uwezo wa kufanya maamuzi, kutawaliwa na mawazo ya kifo, kujenga tabia ya ukatili, kukabiliwa na hasira na kukata tamaa.

Nyingine ni mhusika kujihisi amepoteza hali na haki ya umama, kuwatamani na kuwapenda watoto wa wengine, kutamani kuvunja mapenzi, kukosa uwezo wa kusamehe na kujihisi kunyonywa.

Ukweli ni kwamba hata mwaname anayesababisha au kushiriki vitendo vya utoaji mimba hupata laana hizo moja au zaidi. Kiimani, Mungu hutamka laana kwa njia ya dhamiri zetu na laana hizo hufuatiwa na adhabu ambazo nyingine zinaweza kudumu katika maisha yote ya mhusika. Kutoa mimba ni kuua ndiyo maana hata sheria za nchi mbalimbali zinaweka adhabu kali kwa kosa hilo.

Kiimani anayemwua mwingine katika dhamiri yake anaisikia ile laana ya Mungu ikitamkwa waziwazi: Umelaaniwa wewe.” Kisha, anakabiliwa na adhabu zinazomsabishia mateso, maumivu, majuto na huzuni.

Laana ya utoaji mimba hujitokeza katika maumbo na matendo mbalimbali na kwa watu mbalimbali. Iko laana anayoipata mwanamke mtoaji mimba; inayowapata watoto wanaosalimika katika jaribio la kutoa mimba au waliozaliwa kabla au baada ya mwenzao kuuawa, au watoto waliozaliwa katika nchi iliyopitisha sheria ya utoaji mimba. Aidha, ipo laana inayompata daktari au mtu yeyote aliyemwua mtoto kabla hajazaliwa.

LAANA KWA MWANAMKE

Tuangalie kwanza laana katika muktadha wa Biblia Takatifu ili tuone jinsi inavyohusiana na laana ya utoaji mimba. Laana hutolewa/ hutamkwa na Mungu baada ya mwanadamu kukiuka amri au maagizo yake.

Huambatana na adhabu inayoweza ama ya kimwili, kisaikolojia au kiroho.

Laana ya kwanza

Wanazuoni wanagawa laana hiyo katika makundi ya muda mfupi na muda mrefu. Hebu tuangalie laana hiyo katika mtazamo wa kisa cha Kaini na Abel.

Kwa kumwua mtoto wake mwanamke anatoa kafara ya mtoto wake na damu yake kuwa chakula cha Ibilisi. Mungu anamwambia Kaini ‘damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi’.

Kumbe damu ya mtoto anayeuawa inamwagika ardhini na maiti ya mtoto aliyeuawa inatupwa ardhini na hivyo kuwa ndicho chakula cha ibilisi. Idadi ya wanawake watoaji mimba inapoongezeka, ndivyo ibilisi anavyojipatia chakula kwa wingi.

Kumbuka kila tendo la utoaji mimba, mwanamke anamwaga damu yake; na mtoto siyo tu anamwaga damu, bali pia mwili wake. Hivyo, ibilisi anajilisha kwa damu itokayo kwa mama, damu na maiti ya mtoto aliyeuawa katika mauaji hayo.

Kilele cha ushindi wa Ibilisi ni pale nchi inapofikia hatua ya kutunga sheria za kuwaua watoto kabla ya kuzaliwa. Pengine ibilisi anahusisha vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya watoto na vuguvugu la wanawake kudai haki zao; wengine wanaposema kutoa mimba ni moja ya haki juu ya miili yao au ni uhuru wa uchaguzi. Zipo lugha tamu zinazotumiwa kuhalalisha vitendo hivyo viovu kama ‘haki ya afya ya kizazi’ na ‘uzazi wa mpango.’

Laana ya pili

Utoajimimba unahusisha matumizi ya nguvu katika kupanua shingo ya kizazi ambayo baada ya kupata ujauzito, ilifunga ili kumlinda mtoto hadi siku ya kujifungua.

Matumizi haya ya nguvu yanayohusisha vifaa visivyo na vionjo hufanya shingo ya kizazi kulazimika kufunguka na hivyo, kwa vile ni kitendo kilicho kinyume na utaratibu wa nguvu za maumbile, shingo ya kizazi hulegea na haitafungika tena kufikia ukamilifu wake.

Hali hiyo inasababisha mimba zinazofuatia kutoka zenyewe. Ni laana iliyoje kuona watoto wanaofuatia baada ya mwenzao kuuawa, wanachopoka wenyewe kutoka tumboni kutokana na kulegea na uharibifu wa viungo vya kizazi vya mama yao; tena alivyoviharibu wakati akimuua ndugu yao. Huu ndio mwendelezo wa laana kufuatia laana ya kumwua mtoto asiyekuwa na hatia na ambaye hana nguvu ya kujitetea.

Laana ya tatu

Utoaji mimba unahusisha kuingizwa katika viungo vya kizazi vifaa ambavyo havijali ubinadamu wa mtu. Vifaa hivyo vinavyoingizwa kwa nguvu kwa kusukuma na kuvuta huweza kusababisha michubuko na majeraha katika viungo vya kizazi na hivyo kusababisha hatari ya kupata majeraha yasiyopona na hii ndiyo saratani ya shingo ya kizazi.

Mimba inapotungwa, mama huanza kuandaa maziwa katika matiti yake ili kumnyonyesha mtoto. Kama uhai wa mtoto umekatishwa ghafla, maziwa huharibika na kutengeneza sumu inayoshambulia matiti ya mama na kusababisha saratani ya matiti. Mwanamke aliyepata saratani kama hajapata matibabu ya mapema anaendelea kuteseka kadi kifo chake.

Baadhi ya tiba huhusisha kukata matiti ili kusalimisha uhai wa mama. Kwa vyovyote vile, hakuna daktari anayeweza kukata shingo ya kizazi, na hali hiyo husababisha vifo kwa wanawake wengi.

Laana ya nne

Yawezekana vitendo vya utoaji mimba vikaharibu mfumo wa uzazi, au kwa kuchana mfuko wa kizazi na hivyo kulazimika kuutoa wote na hivyo mwanamke huyo hawezi tena kupata ujauzito.

Katika vitendo vya utoaji mimba yawezekana mwanamke akavuja damu nyingi hadi kifo; au pengine katika utoaji mimba mishipa ya fahamu ikaharibiwa na hivyo kumsababishia mwanamke kifo.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania. Anapatikana kwa 0713609641.

Chanzo: habarileo.co.tz