Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa nini wagonjwa wengi wa akili wanatokea Uru?

44712 Pic+kichaa Kwa nini wagonjwa wengi wa akili wanatokea Uru?

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Kumekuwa na hisia na pengine maneno mengi katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Moshi pale anapoonekana mgonjwa wa akili, wao hudai kuwa anatokea maeneo ya Uru wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mji wa Moshi unaonekana kuwa na wagonjwa wengi wa akili wanaozurura mitaani, wengine wakiokota makopo au vyakula kwenye mashimo ya taka wengine wakitembea huku wakirusha ovyo mawe.Wataalamu wanadai ugonjwa wa afya ya akili ni miongoni mwa magonjwa yaliyotajwa kuendelea kushika kasi mkoani Kilimanjaro, huku waathirika wakubwa wakiwa vijana.

Kama ugonjwa huo hauchagui eneo alikozaliwa muathirika, watu wanahoji ni kwa nini maeneo ya Uru yanatajwa kukithiri kwa wagonjwa wengi? Wapo pia wanaouhusisha ugonjwa huo na ushirikina.

Takwimu zinasemaje?

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, daktari wa maradhi ya akili wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, Engelbertus Mafikiri alikiri Uru kuwa na wagonjwa wengi wa akili.

Hata hivyo, daktari huyo alisema licha ya kuonekana wagonjwa wanaougua maradhi hayo wanatoka eneo la Uru, alipinga kuuhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina kama hisia zilivyojengeka miongoni mwa watu.

Dk Mafikiri anasema Hospitali ya Mawenzi inapokea wagonjwa wa akili kutoka mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini.

Kwa mujibu wa Dk Mafikiri, eneo la Uru linaongoza mkoani Kilimanjaro likifuatiwa na Oldmoshi na Kibosho, huku mkoa wa Arusha ukiongozwa na eneo la Usariver.

Anasema mwaka 2018, wagonjwa wa akili waliolazwa hospitalini hapo walikuwa 904, wanawake 388 na wanaume 516 huku waliotokea Uru wakiwa 89.

“Ukiangalia takwimu kulingana na watu walivyoandika mahali wanapotokea, unaweza usione kama Uru inaongoza kwa vile wagonjwa wengi tunaowapokea tunaandika wanakoishi. “Lakini ukifuatilia asili yake alikozaliwa, ndipo huwa tunabaini ukweli kwa sababu mtu mwingine anakuja anakuambia ametokea Arusha, Rombo au kwingine,” alieleza na kuongeza zaidi: “Katika kumchunguza ili kujua tatizo lilikoanzia ndipo tunabaini ametokea Uru.”

Dk Mafikiri anaeleza kuwa visababishi vya maradhi hayo vipo vingi na miongoni wa hivyo ni kurithi, matumizi ya dawa za kulevya, msongo wa mawazo, maradhi kama ya Ukimwi na matatizo ya kifamilia.

Alisema matumizi ya dawa za kulevya na ugonjwa wa Ukimwi, vinaongoza kusababisha kuongezeka kwa ugonjwa huo wa akili, lakini kwa upande wa Uru, sehemu kubwa husababishwa na kurithi.

“Katika eneo la Uru, ugonjwa huu unaonekana ni wa kurithi na wengi huzaliwa nao, na hakuna uhusiano wowote na imani za kishirikina kama vile ambavyo wengi wamekuwa wakidai,” alisema.

“Wagonjwa wengi wa Uru ukifuatilia historia yao utabaini kwenye ukoo alikotoka, ana ndugu waliowahi kuugua kichaa,” amebainisha.

Dk Mafikiri pia alisema kwa upande wa Arusha, tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa za kulevya na waathirika wakubwa ni vijana.

Wenyeji wa Uru wanena

Mkazi wa Uru Kishumundu, Evaristi Ivo alipozungumza na Mwananchi alikiri kuwapo kwa wagonjwa wengi wa akili katika maeneo yao na kudokeza kuwa wengi wanapata tatizo hilo wanapokwenda mjini. “Wengi wanapata tatizo hilo baada ya kutoka nyumbani na kwenda mjini na hili limekuwa likihusishwa na imani za kishirikina.

“Mtaani kwetu kuna wagonjwa kama wanane ninaowafahamu mimi na wanatoka Mwasi, Kishumundu, Mnini na Mawela.

“Hawapati tatizo wakiwa nyumbani. Wakisafiri kwenda Moshi mjini kutafuta kazi au kusoma, wakirudi wanakuwa na ugonjwa huo na wengine wanadaiwa kuwa wamefanywa hivyo na ndugu zao ili wapate mali,” alidai Evaristi.

Diwani wa Rau katika Manispaa ya Moshi, Peter Kimaro ambaye ni mwenyeji wa Uru, alipinga madai ya Uru kuwa na wagonjwa wengi na kueleza kuwa wagonjwa hao wapo maeneo mbalimbali nchini.

“Hapa mjini wagonjwa hawa wanaonekana ni wengi kutoka Uru kwa kuwa eneo hilo ni karibu na mjini na kawaida ya hawa wagonjwa ni kukimbilia mjini kutafuta vitu vya kula.

“Wapo wengine wanatokea maeneo ya Kibosho na maeneo mengine, lakini kwa vile Uru ni karibu na mjini, wanasema ni wa eneo hilo. Ni dhana potofu kudai kila mgonjwa ametoka Uru,” alisema.

Kimaro alipinga pia madai kuwa wanaougua ugonjwa wa akili wamerogwa na ndugu zao na wengine wanadai ni kutokana na kusoma sana, jambo alilosema halina ukweli hata chembe.

Madaktari waeleza wanavyopigwa

Pamoja na jukumu zito la madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mawenzi kuwahudumia wagonjwa wa akili, lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi pamoja na kupigwa. “Tunapigwa sana na wagonjwa, tunang’atwa na kujeruhiwa vibaya. Kwa kweli tunafanya kazi katika mazingira hatarishi sana lakini hatuna hata posho ya mazingira hatarishi,” anasema Dk Mafikiri.

Anasema hata miundombinu ya wodi za wagonjwa hao katika hospitali hiyo si rafiki, hazina milango ya dharura ya kutokea pindi daktari anapovamiwa na mgonjwa akiwa ofisini kwake.

“Kukosekana milango ya dharura ni jambo linalochangia tupigwe na kujeruhiwa na wagonjwa,” anasema Dk Mafikiri huku akimuonyesha mwandishi mazingira ya wodi hiyo.

Anasema changamoto nyingine ni upungufu wa dawa za wagonjwa wa akili jambo linalosababisha ndugu wawatelekeze wagonjwa wao na kuibebesha mzigo hospitali.

“Dawa za wagonjwa hawa zina gharama, wengi wanaokuja wanatoka familia duni, ndugu wakiandikiwa dawa kwenda kuzinunua, wanaondoka na kuwatelekeza wagonjwa.

Amesema ili kuondokana na tatizo hilo, kunahitajika elimu ya kutosha kwa jamii kusudi ielewe kuwa ugonjwa huo upo na ni kama maradhi mengine.



Chanzo: mwananchi.co.tz