Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuwa na nguvu za kiume ni kitu kimoja na uwezo wa kutungisha mimba ni kitu kingine

72841 NGUVU+PIC

Mon, 26 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna muhimu ambacho wanaume wanapaswa kukijua; pamoja na kuwa na nguvu za kiume na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu, bado wanaweza kushindwa kuzaa.

Tatizo hilo linachangiwa na sababu mbalimbali kama nitakavyoeleza kwenye makala haya.

Hivyo kabla sijaendelea nawashauri wanaume wote waliopo kwenye mahusiano au ndoa ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakisumbuliwa na hali ya kutowapa wake zao ujauzito, kabla ya kuwatupia lawama wenzi wao, wanapaswa kupima afya ili kutatua tatizo kwanza.

Nikumbushe tu kuwa kwa enzi tulizonazo sasa, kumlaumu mwanamke kuwa hazai bila mwanaume naye kupima, kijamii inachukuliwa kama ni unyanyasaji wa kijinsia na ni kuendekeza utamaduni wa kizamani.

Sababu ya kwanza ni aina ya maisha ya mwanaume na historia ya utumiaji wa baadhi ya dawa. Dawa hizo zinaweza kuwa za matibabu au za kulevya. Kati ya wanaume walio hatarini kupoteza uwezo wa kuzaa ni wale wenye tabia ya ulevi. Ulevi sio tu unaathiri nguvu za kiume, pia unadhoofisha uzalishwaji stahiki wa mbegu za kiume.

Pia unaathiri mbegu zinazozalishwa kwa kuzifanya zikose afya ya kurutubishwa. Uvutaji igara na bangi, unywaji pombe na hasa wa kupindukia, utumiaji wa dawa nyngine haramu za kulevya unaathiri moja kwa moja uwezo wa kutungisha mimba.

Pia Soma

Lakini hata uzito uliopitiliza pia unaathiri utungishwaji wa mimba. Mwanaume anashauriwa kudhibiti uzito wa mwili ili kudhibiti mafuta ya ziada ambayo kwa kawaida yanaathiri uzalishwaji wa mbegu za kiume.

Matatizo katika utokaji mbegu za kiume ni sababu nyingine iliyo nyuma ya tatizo hili. Haijalishi kama mwanaume ana nguvu za jinsia kwa kiasi gani.

Ujazo wa mbegu za kiume pia ni muhimu katika kufanikisha utungishwaji wa mimba.

Wapo wanaume wachache wanaosumbuliwa na tatizo la mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ambako ndiko zinakotengenezwa na kuchujwa na kwenda kwenye uume. Miirija hiyo huziba kutokana na matatizo mengine ya kiafya kama vile kuwa na mafuta yaliyozidi mwilini, matatizo ya kisukari na hata maambukizi mengine kwenye mfumo wa uzazi.

Hali hiyo ikitokea inatengeneza tatizo jingine ambalo kitaalamu linaitwa ‘sperm motility problem’. Kama kiwango cha mbegu za kiume ni hafifu haziwezi kusafiri kwa kasi inayohitajika hadi kwenye yai la mwanamke kwa ajili ya urutubishwaji kama inavyotakiwa.

Baadhi ya matatizo yanayoweza kuchangia ni kama vile kutokuwa na uwiano wa mfumo wa homoni mwilini, magonjwa au maambukizi kwenye via vya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla, baadhi ya magonjwa ya kurithi, na utumiaji wa baadhi ya dawa ambazo zina mchanganyiko mkubwa na kemikali.

Ili kutambua sababu nyingine zinazoweza kufanya ashindwe kutungisha mimba, mwanaume anapaswa kuwaona wataalamu wa afya ili kupewa msaada zaidi na kutatua tatizo linalomkabili pasipo kujua badala ya kuendelea kumtupia lawama mwezi wake wa kike.

Chanzo: mwananchi.co.tz