Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kutonyonyesha mtoto kunasababisha saratani ya matiti

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uelewa mdogo kuhusu saratani ya matiti umetajwa kuwa sababu ya wanawake kuchelewa kufika hospitali hivyo kupelekea ugonjwa huo kuwa tishio nchini.

Sambamba na hilo pia imeelezwa kuwa sababu nyingine inayochangia kupata ugonjwa huo ni tabia ya wanawake kutonyonyesha mara baada ya kujifungua pamoja na ulevi uliopindukia.

Takwimu zilizotolewa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata) zinaonyesha kuwa saratani ya matiti ni ya pili kwa kuua hapa nchini ikitanguliwa na ile ya shingo ya kizazi, huku duniani ikiwa ya kwanza.

Akizungumza leo Februari 2,2019 katika kuelekea maadhimisho ya siku  ya saratani duniani ambayo huazimishwa Februari 4,  mwakilishi wa Mewata,  Dk Celina Mathias amesema saratani ya matiti ni tishio hapa nchini na inahitaji kutolewa uelewa mpana ili wananchi wengi wahamasike kupima na kuibaini ikiwa katika hatua za awali.

Amesema wagonjwa wengi hufika hospitali saratani hiyo ikiwa katika hatua za mwisho hivyo kuwa ngumu kuitibia kwa mafanikio.

"Tumeamua kufanya uchunguzi huu kutokana na tishio la saratani ya matiti inayotokana na kukosekana kwa elimu,  wagonjwa wengi huanza kupata matibabu wakiwa hatua mbaya ilihali ni rahisi kujichunguza wewe mwenyewe kama una dalili za ugonjwa huo," amesema Dk Mathias.

Amesema saratani ya matiti ikiwahiwa matibabu yake yanakuwa na mafanikio na inatibika kabisa. "Mewata inarudisha  kwa jamii utaalamu ambao wameupata mojawapo ni kutoa vipimo vya aina hii," amesema na kuongeza.

Dk Mathias pia alishauri njia mojawapo ya kupunguza ugonjwa huo ni kunyonyesha na kwamba kutokunyonyesha ni mojawapo ya sababu za kupata ugonjwa huo.

"Kina mama wengi huacha kunyonyesha baada ya kujifungua ama kunyonyesha kwa muda mfupi, uvutaji sigara, unywaji pombe kupita kiasi, haya huchangia kupata aina hii ya " amesema Dk Mathias.

Naye Dk Lulu Sakafu amesema mgonjwa wa saratani ya matiti anaweza kupata tiba na kupona kabisa hivyo hakuna haja ya kuogopa.

"Isipokuwa jambo la msingi ni kuwahi kubaini na unaweza kufanikiwa hilo kwa kupima mara kwa mara na ikibainika unayo katika hatua za awali matibabu yake yanakuwa na mafanikio zaidi" amesema Dk Sakafu.

"Hata kina baba wanapaswa kujua jinsi ya kujichunguza kama wana dalili za ugonjwa huu, kwa sababu umekuwa tishio na wengi kutokana na kuwa na elimu ndogo ya kupima na kujichunguza huibaini ikiwa hatua za mwisho,’’ amesema Dk Sakafu.

Naye Ditrucce Luoga aliyefanyiwa vipimo vya ugonjwa huo amesema kwa elimu aliyoipata atakuwa na uwezo wa kuwafanyia wanaye na kuwaelimisha wanafamilia.



Chanzo: mwananchi.co.tz