Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Kupima watoto DNA kuna madhara makubwa’

5be830da0c7a2b238bb1620f19628be0.jpeg ‘Kupima watoto DNA kuna madhara makubwa’

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANASAIKOLOJIA na wataalamu wa masuala ya ustawi wa Jamii wanashauri jamii kuwa masuala ya kupima kina saba (DNA) ili kujua uhalali wa mtoto au watoto lisiwe jambo la kukimbilia kwa sababu lina madhara makubwa kuliko faida na iwapo italazimu kufanya, wahusika wawe tayari kupokea na kubeba matokeo ya vipimo.

Akizungumza na HabariLEO, Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk Joyce Nyoni alisema katika familia masuala ya kufanya DNA kwa watoto yanapaswa kutazamwa kwa jicho pana zaidi kwa sababu madhara yake ni makubwa kuliko faida.

“Watoto ni kiunganishi cha familia,watoto au mtoto baba anajenga bondi na watoto, amewapa jina lake na mengine mengi ya kuimarisha uhusiano baina yao, sasa ghafla unafanya DNA unajua mtoto sio wako, baadhi ya wanaume wanaweza kuhimili na kuendelea kuishi naoi la wengine hawawezi kuvumilia, hapo ndio mwanzo wa kuparaganyika,”alisema Dk Nyoni.

Alieleza kuwa jambo hilo la kupima na kubaini mtoto au watoto sio wa baba husika linavunja uhusiano baina ya familia na watoto wakishajua huyo sio baba yao huwanyima rah ana kuanza msongo wa mawazo huku baba aliyebaini akiondoka na maumivu makali.

“Ushauri wangu ni kwamba suala la kupima DNA libaki kwenye masuala ya uhalifu na mambo ya mirathi ila kama baba anataka tu kuwapima watoto kutaka kujua uhalali wao, sishauri hilo, kwa sababu madhara ni makubwa, tubaki na utaratibu wetu za zamani kitanda hakizai haramu,”alisema Dk Nyoni.

Alitoa mfano na kusema zipo familia ambazo mke na mume wameoana na wamekaa kwenye ndoa miaka mingi bila kupata watoto na ikatokea mwanamke akachepuka na kupata ujauzito bila mumewe kujua akalea mimba hadi mtoto akazaliwa na wengine wakaendelea kuzaliwa kwa njia hiyo huku mwanaume akiwalea na ikabainika kuwa mwanaume hakuwa na uwezo wa kuzalisha, lakini yote hayo yakabaki siri ya familia.

“Ndio maana nasema hili jambo liangaliwe kwa jicho pana iwe uamuzi wa mwisho kabisa kuchukuliwa, hivi mtoto umeshampa jina lako na umetengeneza bondi na watoto, ghafla unapima unakuta watoto sio wako, utawanyangánya jina lako? Hapo watoto ni wakubwa wanajua unafikiri wanaishi kwa amani hapo au wataondoka, mkeo naye ataendelea kuwa na wewe au mausiano ndio yanavunjika,”alisema Dk Nyoni.

Alisema njia bora ni kubaki kwneye ile Imani na kanuni ya zamani kuwa kitanda hakizai haramu ili kuondoa mkanganyiko huo vinginevyo iwapo baba ameakua kupima akubaliane na matokeo ya vipimo bila kuleta madhara kwa familia.

Alisema suala la kupima DNA libaki kwenye masuala ya mirathi na makosa ya kiuhalifu na jamii isipende kukimbilia jambo hilo kwa sababu pamoja na kuujua ukweli, halina afya katika familia.

Mwanasaikolojia, John Shayo alisema wanaume wanakwenda kupima DNA kwa sababu ya ubinafsi na wivu vitu na kwamba mambo hayo husababisha migogoro kwenye jamii.

Shayo alisema, ubinafsi unasababisha mwanaume aamue kupima DNA ili kujiridhisha kama mtoto au watoto ni wa kwake na kwamba wivu unachangia kwa sababu mwanaume anakuwa hajiamini kama mtoto aliyenaye ni wa kwake.

Alisema msukumo kutoka kwa ndugu au marafiki pia huchangie mwanaume atake kupima DNA ya mtoto au watoto kwa kuambiwa kuwa huenda ‘anaibiwa’ na akipima na kukuta kweli si watoto wake mambo mabaya huibuka kwenye familia.

Shayo aliwataka wanaume wachukulie kawaida taarifa za DNA zinaposema si watoto wao kwa kuwa iwapo wakitaharuki hali inaweza kuwa mbaya kwao kiafya na kwa familia zao.

Alisema miongoni mwa madhara baada ya kupima na kubainika kuwa mtoto si wa baba husika ni sonona na hata matukio mengine mabaya.

Aliwasihi wanajamii wawe waaminifu katika ndoa zao na waepuke kuzaa nje ya ndoa, waache uzinzi na wakishindwa hayo watumie kinga.

Mkazi wa Temeke- Dar es Salaam, Juma Mwahungu alisema, upimaji wa DNA kwake si lazima kwa kuwa kama akibainisha kuwa mtoto au watoto si wake familia inaweza kuvurugika na kusababisha matatizo zaidi.

“Wewe shida yako nini mpaka utafute DNA? Halafu ukishathibitisha?...hili ni suala la saikolojia, zamani wazee walikuwa hawahoji kuhusu watoto, walikuwa hawataki stress na ndio maana walikuwa hawapati magonjwa ya moyo”alisema Mwahungu.

Mwananchi huyo baba wa watoto wanne alisema yeye anaamini watoto wote ni wake na kuwa hata kama wapo au yupo ambaye si wake yeye anatambua kuwa ni wake kwa kuwa wamezaliwa kwenye tumbo la mkewe.

“Najua hili suala linachanganya sana, sasa kama ninaenda kupima DNA na ninaambiwa kuwa mmoja siyo wangu hapo si ndiyo familia inaingia matatizoni, kinachotakiwa ni kujiamini kuwa watoto wote wako na kuwachukulia kuwa ni sawa siyo kuanza kutafutana uchawi”alisema Mwahungu.

Mkazi wa Bombambili Songea, Ally Salehe alisema, kupima DNA ni ushamba na kutojiamini kuwa watoto ni wako.

“Kwanza kuna msemo usemao kitanda hakizali haramu, sasa hapo unataka nini tena kwenda kuhakikisha kama mtoto wao…watu wanahangaika na DNA za nini? Kutafuta stress tu”alisema na kuongeza;

“Kama unampenda na ni mkeo au hata ni mpenzi tu huna haja ya kujichanganya kuanza kupima pima, kwanza hata ukijua kuwa siyo wako ndiyo ili iweje, huyo ni mke wako na kama aliteleza akazaa nje pengine ujue au usijue huyo aliyezaliwa ni ndugu ya wanao,

Hapa namaanisha kuwa usijihangaishe na DNA wewe tunza watoto wote wa kwako na hata wa mkeo kwa kuwa kwanza unakuwa umeshawalea wote hivyo ukihisi kuwa kati ya wanao yupo asiye wako fungamacho endelea na kutunza wote.”

Mkazi wa Tabata kwa Bibi, Ilala- Dar es Salaam, Hamza Mwalela alibainisha kuwa anaweza kupima DNA iwapo akiletewa mtoto wa nje ya ndoa yake kwa maana kama akiletewa mtoto na mwanamke aliyewahi kutembea naye kabla au hata baada ya kuoa, lakini hawezi kuthubutu kupima DNA kwa watoto wa ndani ya ndoa.

Alisema, kama kukiwa kuna uhitaji wa kutakiwa kumsomesha mtoto huyo au kumpatia matunzo ya aina yoyote ndiyo atakubali kupima DNA ili kujihakikishia kuwa anayemtunza ni mtoto wake.

Alisema mbali na hapo hatokaa kupima DNA huku akiwataka watu kuacha kupima pima DNA kwa kuwa inaweza kuwa mwanzo wa matatizo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz