Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kukosekana huduma ya upasuaji kulivyoondoa uhai wa mjamzito

33384 Pic+upasuaji Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunduru. “Nimempoteza binti yangu akiwa na ujauzito wa miezi minane na wiki mbili kwa kukosekana huduma ya dharura ya upasuaji katika zahanati ya kijiji chetu (sasa kituo cha afya) Mkasale wilayani Tunduru”.

Hivyo ndivyo alivyoanza kuzungumza Mwajuma Omary 54 mkazi wa Kijiji na Kata ya Mkasale, Tunduru mkoani Ruvuma akielezea athari za kukosekana kwa huduma ya upasuaji katika kituo hicho cha afya na kusababisha madhara mbalimbali.

Anasema mwanae Fatma Awadhi (26) amemwachia jukumu zito la kulea wajukuu wawili ambao sasa wanamtegemea yeye wakati awali yeye mwenyewe alikuwa akihudumiwa na mtoto wake huyo kwa kila kitu.

“Nilimtegemea mwanangu anihudumie lakini ameondoka kwa kukosekana huduma ya upasuaji. Sasa nimekuwa tegemeo la pekee kwa wajukuu zangu kwa chakula, mavazi na mahitaji muhimu ya shule.

“Siku aliyofariki mvua kubwa ilinyesha na binti yangu aliamka akiwa na afya njema, alifanya usafi chumbani kwake na kupata kifungua kinywa, lakini baada ya muda aliniita akaniomba nimsaidie kuchunguza kwani alihisi maumivu makali ya tumbo,” anasema.

Anasema alipomkagua aligundua tayari chupa ya uchungu ilikua imevunjika, hivyo kwa kushirikiana na majirani walimbeba na kumkimbiza kituo cha afya.

“Tulihangaika kumbeba kwenye kitanda cha kamba. Alionekana kuwa na kifafa cha mimba. Hata hivyo, baada ya kufika zahanati (sasa kituo hicho), daktari alituambia kuwa hawana uwezo wa kumtibu na kututaka tumuwahishe Hospitali ya Wilaya Tunduru kwa ajili ya upasuaji,” anasema.

Mwajuma anafafanua zaidi kuwa hali ya mwanae ilizidi kuwa mbaya, walimfikisha hospitali ya wilaya kwa pikipiki lakini wakati ndugu wakichangia damu kwa ajili ya kumnusuru huku wauguzi wakimuandaa mgonjwa ili apelekwe chumba cha upasuaji mwanae alifariki.

“Niliumia sana. Nimepitia magumu mengi, sasa ni miaka mitatu tangu nimpoteze mwanangu na kiumbe chake kilichokuwa tumboni angalau nimefarijika kuona Serikali imesikia kilio cha wananchi na kuamua kuipandisha hadhi zahanati yetu na kuwa kituo cha afya. Pia kwa kuamua kutujengea chumba cha upasuaji kwa ajili ya wajawazito na maabara, hatua hiyo itatuhakikishia kupata huduma muhimu za matibabu,” anasema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Salum Chipaka anasema ukosefu wa chumba cha upasuaji kwa wajawazito katika kituo hicho cha afya umechangia wajawazito kupoteza maisha au vichanga vyao kwa kukosa huduma muhimu hasa za dharura.

Anasema kutokana na changamoto hiyo, Serikali imetoa zaidi ya Sh700 milioni kwa ajili ya upanuzi na uboreshwaji wa kituo hicho cha afya ikiwamo ununuzi wa vifaa tiba, hivyo adha ya kujifungulia njiani au kwa waganga wa jadi itaondoka na hivyo kupunguza vifo wajawazito na watoto.

Naye Amina Ally mkazi wa kijiji hicho, anasema anaamini hali ya huduma ya afya kijijini kwao na maeneo ya jirani itaimairika baada ya kuboreshwa kwa kituo hicho.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Wendi Robert anasema ujenzi wa kituo hicho ulianza rasmi Januari 30, mwaka huu na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 ili kianze kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 4,000.

Anasema wamepokea Sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi na Sh300 milioni za kununulia vifaa tiba na dawa ili kituo kitakapokamilika kianze kutoa huduma mara moja.

Anataja baadhi ya changamoto wanazokutana nazo ni upungufu wa watumishi ambapo anaiomba Serikali kuhakikisha inapeleka watumishi wa kutosha akiwemo daktari ili kuwasaidia wananchi. “Kituo hicho kinakabiliwa na upungufu wa watumishi na hakina mganga”.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, alieleza kuridhishwa na hatua za ujenzi huo na kuagiza kamati ya ujenzi na mafundi kujitahidi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Homera anasema waliokabidhiwa jukumu la usimamizi watumie vyema fedha zilizotolewa ili fedha zitakazobakia ziweze kufanya ukarabati wa majengo ya zamani.

Majengo yanayojengwa ni la chumba cha kujifungulia, wodi ya watoto, chumba cha upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti na maabara.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk Gozberth Mutahyabarwa, anasema tatizo la vifo vya wajawazito na watoto bado lipo mkoani humo na kusema juhudi zinazochukuwa zitaboresha upatikanaji wa huduma na kupunguza changamoto hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz