Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kujifungulia nyumbani na hatari ya kuzua magonjwa yasiyoambukiza

372fdbbcec6e276470ad31e779fa0316 Kujifungulia nyumbani na hatari ya kuzua magonjwa yasiyoambukiza

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TABIA ya baadhi ya akina mama kujifungulia nyumbani imekuwa ikisababisha madhara mengi ikiwemo kupata magonjwa yasiyoambukiza mbali na hatari ya vifo kwa mama, mtoto au wote kwa pamoja.

Ni katika muktadha huo, wanawake wajawazito wanahimizwa sana kuhakikisha wanajifungulia kwenye vituo vya afya, hasa kwa kuzingatia kwamba serikali ya awamu ya tano inajitahidi kusogeza vituo vya afya karibu na wananchi.

Hata pale ambao bado vituo vya afya viko mbali, jamii zinashauriwa kuanza kutunza fedha baada ya mwanamke kupata ujauzito ili iwe rahisi kusafiri kwenda karibu na huduma wakati wa kujifungua unapowadia.

Hata hivyo, pamoja na kelele ambazo zimepigwa sana kuwataka akina mama kujifungulia kwenye vituo vyenye watalaamu wa afya na wakunga waliosomea, bado kuna akina mama wachache wanaoendelea kujifungulia nyumbani, baadhi wakitumia njia ambazo siyo za kisayansi na hivyo kuwaletea madhara.

Teddy Tamasha (34) ni miongoni mwa wanawake waliokuwa wakizalia nyumbani, akitumia njia ya kukoroga chumvi kiasi cha nusu kilo na kunywa, akiamini ni tiba ya kuwahisha kutoka kwa kondo la nyuma wakati wa kujifungua. Njia hii sasa inahusishwa na kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya kiafya yanayomkabili.

Tamasha mwenye watoto wanne, mkazi wa kijiji cha Ilobashi, kata ya Masengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga anasema njia hiyo alifundishwa na mama yake alipokuwa mkunga wa jadi, akiitumia kuwasaidia wanawake wengine kujifungulia nyumbani.

“Nimekuwa nikitumia njia ya kukoroga chumvi kwa watoto wangu wote ambao nimejifungulia nyumbani. Kwa vile sikuona madhara yoyote, sikuwahi pia kwenda hospitali. Mwanangu wa wanne sasa ana umri wa miaka minne,” anasema Tamasha.

Hata hivyo, anasema katika siku za karibuni amekuwa akisumbuliwa na magonjwa ambayo siyo ya kuambukizwa na wataalamu wamegundua kuwa na uhusiano na chumvi nyingi aliokuwa akitumia wakati wa kujifungua.

Matatizo hayo anasema ni pamoja na kuvimba miguu na kuumwa sana tumbo hadi kufikia hatua ya kupoteza fahamu na wakati mwingine kulazwa.

“Njia ya kutumia chumvi kiasi cha nusu kilo kwa kuikoroga kwenye maji na kunywa ili kondo la nyuma litoke nimewafundisha watu wengi ambao walikuwa wakijifungulia nyumbani. Wakati huo sikujua madhara yake lakini wengi sasa wanakutana na madhila kama ninayoyapata,” anasema.

Mumewe, Joachim Mussa, anasema hafahamu njia alizokuwa akitumia mke wake kujifungua isipokuwa alikuwa akimkuta tayari ana mtoto.

Kilichokuwa kinatokea anasema mkewe alipokuwa akikaribia kujifungua alikuwa akiondoka nyumbani wanakoisha na kwenda nyumbani kwa wazazi wake kupata msaada wa kujifungua.

Baadhi ya ndugu wa Tamasha ambao wamekuwa wakimuuguza, Violet Charles na Monica Julius, wanasema hawajui chanzo cha ugonjwa wake isipokuwa ndugu yao amekuwa akishindwa kutembea kutokana na kuvimba miguu na wakati mwingine kupata shinikizo la juu la damu hadi kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.

Monica anasema hivi sasa nduguye huyo amekuwa mtu wa kushikiliwa kwa sababu hawezi kutembea mwenyewe, hawezi kubeba ndoo ya maji na wakati mwingine anashindwa hata kuogesha watoto wake zaidi ya kuwa mtu wa kulala muda wote.

Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi, Dk Agustine Maufi, anasema kuzalia nyumbani na kutumia dawa ambazo hazijathibitishwa na wataalamu huweza kumletea madhara mtu ndani ya tumbo, ini moyo na kwenye via vya uzazi.

“Mara nyingi akina mama kama Tamasha wanapougua na kuzidiwa ndipo hueleza walichotumia wakati wa kutoa mimba au kuondoa kondo la nyuma na hasa matumizi ya dawa za kienyeji ambazo wengine wamekuwa wakikutwa nazo wakitumia kwa usiri mkubwa hata wanapoletwa hospitalini kujifungua,” anasema Dk Maufi.

Dk Maufi anasema baadhi wamekuwa wakija kujifungua wakiwa na dawa ambazo wanaamini zitaharakisha uchungu ili wawahi kujifungua lakini nyingi ya hizo kama siyo zote zina madhara kwao na wakati mwingine hata kwa mtoto.

Anawaonya akina mama kuacha kutumia dawa ambazo hazijathibitishwa na watalaamu wakati wakiwa na ujauzito hadi wakati wa kujifungua na badala yake wafuate maagizo ya watalamu.

Mratibu wa afya ya uzazi, mama na mtoto kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Evodia Richard, anasema akina mama wanaojifungulia nyumbani wamepungua kwa takwimu zilizopo lakini bado wapo.

Anasema wanaojifungulia nyumbani wamekuwa wakitumia vitu vya ajabu visivyo na maelezo ya kisayansi ili kuweza kufanikisha azma yao ya kuwa salama lakini wengi hupatwa na matatizo ya kiafya wakati wa kujifungua ikiwemo kupoteza mtoto au matatizo hayo huja baadaye.

Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Dk Mameritha Basike, anawahimiza wanawake wajawazito kuhakikisha wanajifungulia kwenye vituo vya afya kwani huduma zipo muda wote na wasijifungulie nyumbani wanakojikuta wakitumia dawa ambazo hazijathibitishwa na ambazo zinaweza kuwaletea madhara makubwa badaye.

Basike anasema mama anapojifungulia nyumbani anaweza kupoteza maisha yake na ya mtoto pale anapokumbana na uzazi pingamizi unaohitaji kufanyiwa upasuaji na ni hatari kwake pia kama atahitaji kuongezewa damu.

Anasema kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba mwaka 2020 takwimu zinaonesha kwamba wanawake waliojifungulia nyumbani katika halmashauri hiyo walikuwa 96 sawa na asilimia 0.7 ya wanawake wote waliojifungua.

Lakini anasema kwa mwaka 2019, wanawake 195 ndio walibainika kujifungulia nyumbani katika halmashauri hiyo, sawa na asilimia 1.24 ingawa idadi hiyo pia imepungua kulinganisha na miaka ya nyuma.

Kupungua kwa idadi ya wanaojifungilia nyumbani anasema kunatokana na uhamasishaji wa kujifungulia kwenye vituo vya afya ambao umekuwa ukifanywa pamoja na hatua ya serikali kusogeza huduma za vituo vya afya na zahanati karibu na wananchi.

Mwaka 2015 utafiti ulionyesha kwamba mkoani Shinyanga asilimia 50 ya wajawazito walikuwa wakijifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi, hali ambayo ilisababisha takribani wajawazito 64 kupoteza maisha kwa mwaka huo pekee kutokana na kukutana na uzazi pingamizi na hatua za kuwakimbiza kwenye vituo vya afya kuchelewa.

Mkurugenzi wa tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Maghembe, anasema takwimu za wizara hiyo zinaonesha kwamba kwa takribani miaka nane sasa magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka katika kutesa kundi la vijana wakiwemo wanawake ambao wanajifungulia majumbani.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, (Muhas), Profesa Andrea Pembe anasema matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza katika jamii yameongezeka hadi kufikia kati ya asilimia 18 hadi 30 ya magonjwa yote wakati miaka ya 1960 matatizo hayo yalikuwa ni wastani wa asilimia moja tu.

Chanzo: habarileo.co.tz