Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuchelewa kula usiku hatari ya kupata kisukari

89320 Chakula+pic Kuchelewa kula usiku hatari ya kupata kisukari

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watu wanaochelewa kula chakula usiku wapo katika hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari.

Ofisa Lishe Mwandamizi, kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC) Adeline Munuo anasema: “Usiku mtu anashauriwa kula mapema halafu akae saa walau mbili ndiyo akalale na si kula tu na kwenda kulala, kama unalala saa tatu, basi unatakiwa saa moja usiku uwe umeshakula chakula.”

Anashauri usiku watu wapunguze kula vyakula vya wanga kama wali au ugali, badala yake wajikite kula mboga mboga na matunda.

“Asubuhi unaweza kula chakula kizito kwa sababu mwili utaushughulisha na mazoezi ya kutembea na kufanya kazi nyingine, lakini usiku watu wanakula chakula na kulala.

“Hapo mwili haupati muda wa kufanya mazoezi, hivyo ndiyo maana tunashauri mlo wa usiku uwe mwepesi au kula chakula ambacho kina wanga kwa kiasi kidogo,” anafafanua.

Pia, anasema watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari ni wale wanaokula kupita kiasi na ambao hawafanyi mazoezi kwa maana ya kutembea na kufanya shughuli nyingine.

Munuo anasema kila mtu anapaswa ale mlo kamili unaohusisha chakula mchanganyiko kutoka katika makundi matano ya chakula bila kusahau kufanya mazoezi hata ya kutembea.

Anayataja makundi hayo kuwa ni kundi la vyakula vya nafaka, viazi , mihogo na ndizi.

Lingine ni kundi la vyakula vya jamii ya kunde na vya asili ya wanyama, matunda, mbogamboga, mafuta na sukari.

“Kiwango cha chakula unachokula kinaangalia vitu vyote hivyo, kuanzia umri wako, hali yako ya mwili je ni mzima au ni mgonjwa au ni mjamzito au unanyonyesha? Hivyo kiwango cha chakula unachokula lazima kiangalie hivi vyote,” anasema Munuo.

Chanzo: mwananchi.co.tz