Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kongwa yapata mashine ya watoto njiti

Wed, 14 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kongwa. Wakazi wa Wilaya ya Kongwa wameondokana na changamoto ya kusafiri umbali wa kilomita 85 kutoka wilayani humo hadi Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa ajili ya kupata huduma ya watoto njiti. Changamoto hiyo imekwisha baada ya taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana na Benki ya Diamond Trust (DTB) kutoa mashine ya kuhudumia watoto waliozaliwa kabla ya siku (njiti) yenye thamani ya Sh11 milioni kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kongwa. Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo Mganga mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Magreth Kagashe amesema kuwa hospitali hiyo ilikuwa inapoteza watoto njiti kwa kuwa hawakuwa na mashine ya kuwahifadhi. "Tulikuwa tunalazimika kusafiri umbali wa kilomita 85 kuwapeleka watoto hao Hospitali ya General ambapo hata hivyo wengine walikuwa wanakufa njiani kutokana na urefu wa safari," amesema Dk Kagashe. Ameongeza kuwa hospitali hiyo hupokea wastani wa watoto 13 kila mwezi ambao wamezaliwa kabla ya siku zao na kulazimika kuwasafirisha hadi Hospital ya General kwa uangalizi zaidi. Akipokea vifaa hivyo Spika wa Bunge ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kongwa, Job Ndugai amesema kuwa ni lazima wadau mbalimbali kusaidia makundi yenye mahitaji maalum kwa sababu Serikali peke yake haiwezi kuyafikia makundi yote kwa wakati. Amesema kundi la watoto njiti limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi kwa sababu limesahaulika na kusababisha watoto wengi wanaozaliwa kabla ya kutimiza siku kufa na hata wengine kuishi kwa tabu. Aidha ameomba kujengewa wodi ya wazazi katika hospitali hiyo ambayo itapunguza msongamano wa akina mama wajazito katika hospitali hiyo katika eneo hilo lenye wakazi zaidi ya 350,000. Naye Doris Mollel aliwaomba wahudumu wa hospitali hiyo kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kuokoa maisha ya watoto njiti na kupunguza safari za kwenda Hospitali ya Mkoa Dodoma ambayo husababisha baadhi ya watoto kupoteza maisha wakiwa njiani. Amesema tatizo la watoto njiti ni la kimataifa kwani jumla ya watoto 15 milioni huzaliwa kabla ya wakati ambapo watoto 1 milion hupoteza maisha kwa kukosa huduma muhimu za kuwafanya waendelee kuishi.

Chanzo: mwananchi.co.tz