Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kongamano kujadili jinsi ya kukabiliana na vifo vya watoto njiti laanza

27285 WATOTO+PIC TanzaniaWeb

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kutokana na tatizo kubwa la vifo vya watoto chini ya mwezi mmoja nchini Tanzania, wahudumu wa afya wakiwamo madaktari bingwa wameanza mafunzo kupitia kongamano la kisayansi kwa watoto wachanga ili kuendelea kujinoa namna ya kuokoa uhai wao.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, watoto wengi wanaokufa chini ya mwezi mmoja ni njiti ambapo asilimia 13 hadi 17 ya watoto wote waliozaliwa nchini ni njiti.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru amesema Serikali imekuwa ikiratibu programu mbalimbali za kupunguza vifo vya  watoto wachanga.

Amesema pamoja na programu hizo kusaidia kuleta mabadiliko katika kupunguza vifo hivyo bado zipo changamoto mbalimbali zinazowakabili.

"Niwapongeze tu kwa kufanya mafunzo haya ambayo yataongeza tija katika kutoa huduma kwa watoto wachanga ikiwa fursa hii itatumika ipasavyo," amesema Profesa Museru.

Awali, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto nchini Tanzania, Sekela Mwakyusa amesema kwa mara ya kwanza wameamua kufanya kongamano hilo ili kusaidia katika kukabiliana na vifo vya watoto.

Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya kuadhimisha siku ya mtoto njiti Novemba 17 nia ikiwa ni kupunguza vifo.



Chanzo: mwananchi.co.tz