Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwango cha wanawake kujifungua nchini chapungua - Utafiti

Mimba D Watoto Kiwango cha wanawake kujifungua nchini chapungua - Utafiti

Wed, 8 Nov 2023 Chanzo: Mwananchi

Dar es Salaam. Kiwango cha wanawake kujifungua nchini kimepungua kutoka wastani wa watoto 6.2 mwaka 1991-1992 hadi watoto 4.8 kwa mwanamke mmoja mwaka 2022, utafiti mpya umebainisha.

Matokeo hayo yameonyesha kunapungua huko kunatokana na kiwango cha elimu na hali ya uchumi wa kaya husika.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Mkoa wa Dar es Salaam unaonekana kuwa chini kwani wastani wa kujifungua ni watoto 2.8 huku Mkoa wa Simiyu ukiongoza kwa wastani watoto 6.6 kwa kila mwanamke.

Utafiti huo unatolewa baada ya ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya ‘Tanzania in figures 2021’ kuonyesha kupungua uwezo wa kuzaa kwa wanawake kutoka wastani wa watoto sita 2004/2005 hadi 4.9 mwaka 2021.

Ripoti hiyo ilionyesha uwezo wa wanawake kuzaa nchini umeshuka kwa asilimia 18 ndani ya miaka 17 zikimaanisha kila mwaka mwanamke anapunguza idadi ya kuzaa watoto kwa asilimia moja.

Kufuatia utafiti huo, wananchi wanaoishi maeneo ya Dar es Salaam wametoa maoni yao wakisema ugumu wa maisha ya hali ya kiuchumi ni sababu ya wengi kuishia watoto wawili au watatu, sababu nyingine wakitaja kufuata mfumo wa kimagharibi.

“Gharama ya maisha imekua kubwa, Dar es Salaam ukiwa na familia ya watoto wawili unatakiwa kutumia si chini ya Sh20, 000 kwa siku kwa mahitaji ya kawaida hapo sasa hujampata anayeishi kwa dola moja, hali ni ngumu huwezi kuzaa watoto wengi,” alisema mkazi wa Temeke, Hezron Mwanyeji.

Mwanyeji alisema wanawake wa mijini wengi wanaogopa kuzaa kwa njia ya kawaida hali inayowafanya wengi kukimbilia upasuaji ambao unakuwa na ukomo wa idadi ya watoto.

Mkazi wa Tabata Jenifer Mwansasu alihoji:“Dar gharama ni kubwa kuanzia chakula, mavazi kila kitu na kama hujajenga nyumba, kupanga nyumba nzima ina vyumba vitatu vya kulala na gharama yake iko juu ukiwa na watoto sita utawaweka wapi?”

Kwa upande wa mikoani hali ni tofauti kwani wengi wamesema wamepokea elimu kuhusu uzazi wa mpango, “Nikijifungua ninaelekezwa kuhusu uzazi wa mpango hivyo najikuta naweka vijiti nakaa miaka miwili au mitatu navitoa nazaa tena.”

Mratibu huduma ya afya ya uzazi, mama na mtoto Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu Magreth Mabebe alisema wanawake wa Wilaya hiyo wanazaa watoto wengi.

“Kwa mfano Kata ya Mwaswale ina wakazi wengi, hata uzalianaji unakua mkubwa kwa wiki wanazaliwa watoto 30 na kutokana na ongezeko shule sasa hazitoshi hivyo wanajenga nyingine kukidhi mahitaji,” alisema na kuongeza kuwa wastani wa kuzaa kwa nchi ni watoto watatu mpaka wanne kwa mama mmoja na hivyo wanapambana kutoa elimu ili angalau mama mmoja azae watoto watano kufikia mwaka 2025.

Ripoti ya utafiti

Utafiti umeonyesha wanawake wanaoishi katika maeneo ya vijijini wana uwezo wa kuwa na watoto wengi kuliko wanawake wa maeneo ya mijini kwa wastani wa watoto 5.5 dhidi ya 3.6 mtawalia.

Kimkoa, uzazi unatofautiana kulingana na mkoa husika na kwamba kuna tofauti ndogo ya uzazi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa wastani wa watoto 4.8 ukilinganisha na 4.7 kwa mwanamke.

“Kiwango cha uzazi nchini Tanzania kinapungua kulingana na ongezeko la kiwango cha elimu, kutoka wastani wa watoto 6.3 kwa wanawake ambao hawana elimu hadi wastani wa watoto 3.8 kwa wanawake wenye elimu ya sekondari na zaidi,” umeeleza utafiti huo na kuongeza;

“Aidha, utafiti huu umeonyesha kuwa kiwango cha uzazi kinapungua kadiri hali ya uchumi wa kaya unavyoongezeka. Wanawake wanaoishi kwenye kaya za uchumi wa chini wana wastani wa watoto 6.7 ikilinganishwa na wanawake kutoka kwenye kaya zenye uchumi wa juu wastani wa watoto 3.3.”

Utafiti huo ulifanyika kupitia sampuli wakilishi ya kitaifa iliyohusisha wanawake 15,254 wenye umri wa miaka 15-49 kutoka kwenye kaya 15,705 zilizochaguliwa na wanaume 5,763 wenye umri huohuo walifanyiwa mahojiano.

Mtazamo wa jamii, wataalamu

Wakati lengo la Serikali ni kila mwanamke kuzaa watoto watatu, wataalamu wa masuala ya afya na uchumi wamesema jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali watu wazae kwa mpangilio sasa imeanza kutoa matunda.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) Feddy Mwanga alisema wanawake wengi wamepata elimu ya kuwa na utofauti wa muda kati ya mtoto na mtoto kwa miaka miwili au mitatu hali inayoonyesha elimu imefanikiwa.

“Uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia huduma za uzazi wa mpango, kupanga uzazi ndiyo sababu idadi ya watoto kwenye familia imepungua kwani wameelimishwa kuzaa idadi ya watoto wanaoweza kuwahudumia kwa mahitaji yote muhimu,” alisema Mwanga.

Mkurugenzi wa Miradi, UMATI, Daniel Kirhima alisema matokeo hayo yanaashiria jamii hasa kinababa au familia imejenga uelewa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Kilichokuwa kinachangia zaidi kwanza ni masuala ya tamaduni na kuzaa watoto wengi, wanaume walikuwa wanafikiria ni utajiri wa familia kumbe sivyo, jamii imeanza kuelewa baada ya wadau wengi kufanya kazi na serikali kwa ukaribu kuelimisha jamii kupanga uzazi kwa ajili ya kujenga uchumi,“ alisema.

Kirhima alisema jamii kubwa kwa sasa imekubali matumizi ya njia za uzazi wa mpango wa kisasa hali inayomfanya mwanamke kutumia miaka mitatu mpaka mitano hiyo imesaidia kupunguza idadi ya watoto kwani uelewa ni mkubwa.

“Wadau wa maendeleo hasa sekta ya uzazi tumeweka nguvu nyingi hasa kuelimisha eneo hilo kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha tunafikisha elimu, Umati tumefanya kazi kubwa ya kupita kwa wafugaji na wakulima ambao vituo vyao vipo mbali,” alisema

Alisema kufikisha elimu imesaidia kupunguza pia masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya uchumi na biashara, Oscar Mkude anasema kwa sasa wastani wa kumaliza elimu ya msingi imeongezeka kutoka miaka saba mpaka 10 hiyo itasababisha wengi wachelewe kuingia kwenye uzazi.

“Mipango elimu ya msingi iende mpaka miaka 10 watoto watasoma mpaka kidato cha nne na hiyo itatufanya tufikie lengo la watoto watatu kwa kila mwanamke kutoka 4.8 ya sasa mpaka asilimia 3.

“Familia ya watoto wachache ina uwezekano wa kupata mahitaji yote muhimu kuanzia chakula bora, elimu bora na malezi bora ikilinganishwa na familia yenye watoto wengi,” alisema.

Mkude alisema familia yenye watoto wengi kuliko kipato inalazimika kutumia kwa watoto wengi hivyo ubora wa matunzo hupungua na hiyo inawafanya wasiwe bora na wazalishaji wazuri baadaye hivyo anakuwa tofauti na watoto waliopata mahitaji yote.

“Taifa likiwa na watoto wengi ambao hawakupata malezi bora wanakuwa si wazalishaji na hivyo kushindwa kuchangia kwenye pato la taifa hivyo thamani ya uzalishaji inakuw, na idadi ya watu inapokuwa kubwa na hakuna uzalishaji hakuwezi kuwa na maendeleo kwani wazalishaji wanakuwa wachache,” alisema Mkude.

Chanzo: Mwananchi