Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda dawa za asili kuanza na tezi dume, selimundu

262db77bf61bdc91975d4af29fc5b719.png Kiwanda dawa za asili kuanza na tezi dume, selimundu

Mon, 10 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI inajenga kiwanda cha kuzalisha dawa asili za magonjwa ya binadamu kinachotarajiwa kuanza uzalishaji mwaka huu kwa kuanza na dawa za magonjwa ya selimundu na tezi dume.

Kiwanda hicho kinajengwa katika ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Ubungo External mkoani Dar es Salaam na kitagharimu Sh bilioni 1.5.

Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti wa NIMR, Dk Paulo Kazyoba, alisema kiwanda hicho kilianza kujengwa takribani miaka 10 iliyopita, lakini hakikukamilika na Februari mwaka huu walianza kujenga jengo lingine kwa ajili ya kusimika mitambo.

Dk Kazyoba alisema hadi sasa mitambo ya kuchuja na kukausha dawa imefika kwa ajili ya kuzalisha dawa za magonjwa baada ya taasisi hiyo kuzifanyia utafiti dawa hizo.

Alisema wamenunua mitambo ya uzalishaji wa msingi wa dawa na pia uzalishaji wa hatua ya pili kwa ajili ya utengenezaji wa dawa asili zinazotokana na mimea.

Dk Kazyoba alisema mitambo iliyonunuliwa kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeshaletwa na ipo takribani aina sita na itaanza kufungwa mwezi wa ujao.

“Kwa kuwa mitambo hii ni ya kisasa na mikubwa, itafungwa kwa zaidi ya wiki mbili kisha kufanyika majaribio na kurekebisha changamoto zitakazojitokeza kabla ya kukabidhiwa kwa taasisi,“ alisema.

Kazyoba alisema mitambo hiyo ya kisasa ikishafungwa kutakuwa na mafunzo kwa wafanyakazi waendeleshaji na jinsi ya kuiendesha na mafunzo hayo yatafanyika kwa wiki mbili au zaidi.

Alisema baada ya mafunzo, wafanyakazi wanatakiwa kuzoea uendeshaji wa mitambo ili kupata dawa bora na katika kujihakikishia baada ya kufunga mitambo, ni vema kujipa miezi kadhaa kuangalia kasoro zinazojitokeza.

“Ili kufikia uzalishaji wa dawa bora baada ya kufungwa kwa mitambo na uzalishaji kuendelea ni vema kujipa miezi mitatu hadi sita ndipo uzalishaji wa jumla wa dawa za kuepeleka maeneo mbalimbali utakapoanza,” alisema.

Alisema kiwanda hicho kitazalisha dawa kwa mfumo wa kimiminika na kutengeneza vidonge katika mfumo wa kapsuli.

Alisema utatumika mfumo huo kwa sababu nyingi za utaratibu huo zinaingia tumboni na kupasuka hivyo kutoa tiba madhubuti.

“Utengenezaji wa vidonge tutaanza hapo baadaye kwani mtambo wake haukununuliwa katika awamu hii kutokana na mashine tuliyokuwa tunataka kuwa ya gharama kubwa… Tunatarajia kuanza kutengeneza vidonge kuanzia mwakani mwanzoni,” alisema Dk Kazyoba.

Alisema kwa kuanzia, wataanza na kimiminika kisha kapsuli lakini pia, kuna dawa nyingine zitatengenezwa kwa mfumo wa vifungashio vya majani ya chai ambayo mgonjwa ataweka katika maji ya moto na kunywa.

“Kwa sasa dawa zilizofanyiwa utafiti zitaendelewa kutafitiwa kwani zipo zilizofanyiwa utafiti na kuthibitishwa zikiwa katika mfumo wa kimiminika, hivyo lazima tukitaka kutengeneza katika vidonge au kapsuli au mfumo mwingine zifanyiwe utafiti kuhakikisha ubora unasalia kuwa bora kama ilivyokuwa awali,” alisema Dk Kazyoba.

Alisema mitambo ya awali sita iligharimu takribani Sh milioni 620 na ukiweka na gharama za kulipa taasisi iliyosaidia kuingiza mitambo nchini na bandari pamoja na taratibu nyingine inafikia milioni 700.

Dk Kazyoba alisema pia kuna ujenzi wa jengo jipya lenye sakafu nzito kutokana na uzito wa mitambo itakayosimikwa hivyo gharama

zitaongezeka na kufikia sh bilioni 1.3.

Alisema gharama zinaongezeka kwa ujenzi wa jengo la zamani kwa kufanyiwa mabadiliko ya mfumo wa hewa na mengineyo kwa kuzingatia miongozo inaweza kufikia Sh milioni 150 hadi milioni 200, hivyo gharama za jumla kufikia takribani bilioni 1.5.

Dk Kazyoba alisema dawa watakazoanza kutengeneza ni zile ambazo utafiti wake unakamilika zikiwa katika kimiminika, lakini sasa watafanya kama kapsuli na kimiminika kubaki kutumika kwa watoto.

Alisema wataanza kuzalisha dawa ya selimundu na tezi dume katika kiwanda hicho kutokana na upatikanaji wa malighafi kuwa nafuu kwani katika mfumo wa kiwanda, lazima kuweka mikakati ya kuzalisha mimea tiba.

“Dawa hizo upatikanaji wa malighafi ni nafuu kwani ukiwa na kiwanda kama hicho ni lazima kuwa na shamba la mimea tiba au kuhamasisha wananchi walime mimea hiyo,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz