Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda chaomba msaada kuteketeza dawa za Tsh.bilioni 2

Kiwanda KPI Kiwanda chaomba msaada kuteketeza dawa za Tsh.bilioni 2

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

Kiwanda cha Keko Pharmaceutical (KPI) kimeomba serikali ikisaidie kuteketeza dawa zenye thamani ya Sh bilioni 1.86 zilizoisha muda wake.

Kiwanda hicho kina mpango wa kuongeza uzalishaji wa aina tano nyingine za dawa, hivyo kitakuwa na aina 15 ya dawa zilizo kwenye orodha ya dawa muhimu kwa mujibu wa Mwongozo wa Matibabu nchini (STG).

Mkurugenzi Mwendeshaji wa kiwanda hicho, Betia Kaema alisema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema uteketezaji wa dawa hizo utagharimu Sh milioni 54, lakini pia changamoto nyingine ni ongezeko la kodi kwa baadhi ya vifungashio na vipuri vya mashine za uzalishaji kiwandani.

Alisema kwa sasa kiwanda kinashindwa kuagiza malighafi na vifungashio vya kutosheleza uzalishaji wa miezi mitatu, kuboresha miundombinu ya kiwanda kufikia kiwango cha kimataifa, kuongeza mashine zaidi kupanua uwezo wa uzalishaji na kulipa madeni ya muda mrefu Sh bilioni 12.

Pia, alisema kiwanda hicho kinashindwa kuongeza kiwango cha uzalishaji kutoka aina 10 zinazozalishwa sasa hadi kufikia aina 15 mwakani, kuboresha mazingira na vitendea kazi kwa wafanyakazi na kuteketeza dawa zenye thamani ya Sh bilioni 1.86 zilizomaliza muda wake wa matumizi tangu mwaka 2013/16.

Alisema wakati kiwanda hicho kinaanzishwa miaka 53 iliyopita, kilikuwa kinazalisha dawa aina moja, lakini katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba mwaka jana kinazalisha dawa aina 10.

Alisema dawa hizo 10 zimeidhinishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), zikiwemo za kutibu magonjwa yatokanayo na maambukizi ya vimelea vya bakteria.

Alisema dawa mpya zinazotarajiwa kuzalishwa na kiwanda hicho ni Vitamin C, azithromycin, zinc na antiseptics na disinfectants.

Alisema kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kukidhi mahitaji ya nchi kwa asilimia 100 na kueleza kuwa KPI awali kilikuwa na uwezo za kuzalisha vidonge milioni 1.5 kwa saa 24, lakini sasa kinazalisha vidonge milioni sita kwa saa 24 kwa aina moja kila aina moja ya dawa.

Chanzo: Habarileo