Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali inatarajia kujenga kituo maalumu cha matibabu ya magonjwa ya milipuko Mkoani Kagera, ili kukabiliana na tishio la Ebola kutokana na jiografia ya mkoa huo, ambao umezungukwa na nchi nyingi.
Waziri Ummy, ameyasema hayo wakati wa kikao cha kuhitimisha ziara yake ya kikazi, na kusema Jumuiya ya Kimatiafa inazitaka nchi kujiandaa na majanga, hivyo lazima kuwekeza kwenye ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko.
Amesema, watumishi wa Afya wanatakiwa kuwa tayari kuokoa maisha ya watu pindi atakapopatikana mtu mwenye maambukizi ya Virusi vya Ebola na kuzitaka kamati za usimamizi wa huduma za afya ngazi za Mikoa na Halmashauri kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uelewa watumishi wote kwenye maeneo yao.
Ummy ameongeza kuwa, “Watoa huduma za afya mnao wajibu wa kuokoa maisha ya wananchi hivyo wakati wa kuhudumia kumbukeni kuzingatia kukinga na kudhibiti maambukizi kwako mwenyewe.”
Hata hivyo, amezipongeza kamati kwa utoaji wa huduma na kuzitaka kufanyakazi kwa usimamizi utakaoleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma kwa Wananchi.