Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Profesa Andrea Pembe amesema kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na mishipa ya damu kikikamilika kitakua na uwezo wa kudahili wanafunzi 15,000.
Prof Pembe amezungumza hayo leo Disemba 6, 2021, akiwa Mloganzila jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuongeza mafunzo ya kibingwa.
"Mpaka sasa kimekamilika asilimia 97 kina madarasa, kumbi za semina za kuingiza watu 400, maabara nne za tafiti, ofisi na tayari watalaamu 38 wanapatiwa mafunzo ya kibobezi ya Moyo na mishipa ya damu na kati yao 29 wameshamaliza."Profesa Pembe.
Aidha, ujenzi wa jengo la kituo cha umahiri kwa ajili ya kufundishia, kufanya tafiti za masuala ya moyo na mishipa ya damu na kutoa huduma, ulianza mwezi Februari 2018 na ulitakiwa udumu kwa mwaka mmoja.
“Muda wa ujenzi umekuwa ukiongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ya hewa, changamoto ya Covid-19, changamoto zinazohusiana na msamaha wa kodi kwa vifaa vya ujenzi vilivyosafirishwa kutoka nje ya nchi, na vile vinavyonunuliwa hapa nchini,” amesema Prof Pembe.