Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kituo cha afya Mlandizi kutopanda hadhi

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Licha ya wanawake karibu 10 kujifungua kila siku katika Kituo cha Afya Mlandizi mkoani Pwani, Serikali imesema haina mpango kwa sasa kukipandisha hadhi kuwa hospitali ya wilaya.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Juni 20 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Josephat Kandege wakati anajibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Hawa Mchafu.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itakipandisha hadhi kituo hicho na kuwa hospitali ya wilaya kwa kuwa kimekidhi vigezo.

Naibu waziri amesema kituo hicho hakijakidhi vigezo vya kukifanya kiwe hospitali ya wilaya, hivyo hakuna mpango wowote wa kukipandisha hadhi kama ilivyoombwa.

Amesema Serikali imeamua kituo hicho kiendelee kutoa huduma kama kituo cha afya na badala yake aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali.

“Serikali imeshatenga fedha kiasi cha Sh1.5 bilioni katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya ujenzi huo na tayari halmashauri imeshatenga eneo la eka 32 lililopo kitongoji cha Disunyala kwa ajili ya ujenzi huo,” amesema Kandege.

Kuhusu deni la Sh80 milioni ambalo kituo hicho kinadaiwa, amesema ulipaji wa deni hilo unategemea mapitio kamili ya uchambuzi wa deni.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz