Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisukari, saratani tishio vifo hospitalini

D226055c39870feddf9fda7d4a29e1d2 Kisukari, saratani tishio vifo hospitalini

Mon, 3 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAGONJWA yasiyo ya kuambukizwa yakiwemo ya kisukari, saratani na shinikizo la damu yamechangia kwa asilimia 40 ahdi 45 ya vifo vinavyotokea sasa katika hospitali nchini ikilinganishwa na asilimia 33 kwa miaka mitano iliyopita.

Hayo yamebanishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Profesa Makubi alibainisha kuwa katika kuhakisha idadi hiyo ya vifo inapungua nchini, wananchi wanatakiwa kuzingatia ufanyaji wa mazoezi, kupunguza vyakula vya mafuta, unywaji wa pombe kupitiliza pia kuepuka unene uliopitiliza na kuepuka uvutaji wa sigara.

“Hali ikiachwa kuendelea hivi, itakuwa mbaya zaidi kwa kuwa idadi ya vifo kutokana na magonjwa yasiyo ya kumbukiza ni kubwa na inapaswa kukabiliwa, hivyo mazoezi na kupunguza vyakula vya mafuta na matumizi ya sukari kupita kipimo ni mambo yanayopaswa kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema Profesa Makubi.

Katika hatua nyingine; Profesa Makubi alibainisha kuwa ugonjwa wa ukimwi umeendelea kuwa chini ya asilimia 4.7 huku idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikipungua kwa asilimia 48 kutoka mwaka 2015.

Aidha, maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu yamepungua kwa asilimia 23 huku vifo vikipungua kwa asilimia 33 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Ugonjwa wa malaria wenyewe vifo vimepungua kwa zaidi ya asilimia 60 kati ya mwaka 2015 na 2020.

Profesa Makubi aliwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na kirusi aina ya corona hasa ikizingatiwa kuwa bado unaendelea kuyaathiri mataifa mengine likiwemo taifa la India ambalo kwa sasa linaongoza kwa idadi ya vifo vya kila siku.

Alisema: ”Kwa siku za hivi karibuni, India imekuwa na idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa corona, hivyo kwa kuwa kuna mwingiliano mkubwa wa kibiashara kati ya India na Tanzania, kuna haja ya kuendelea kuchukua tahadhari zaidi, wageni kutoka nchi hiyo inabidi kuendelea kuchukuliwa tahadhari.”

Aliagiza hatua zilizokuwa zikichukuliwa kukabili ugonjwa huo kuendelea kama kawaida huku akihimiza jamii kuendelea kutumia dawa za asili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz