Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio cha watoto wa mjini wazazi kukosa muda nao

82822 Pic+kilio Kilio cha watoto wa mjini wazazi kukosa muda nao

Tue, 5 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Praxseda ni mtoto wa miaka sita anayesoma shule ya binafsi jijini Dar es Salaam na kuna mpango wa kufanya ziara ya kimasomo visiwani Zanzibar.

Lakini huonana na wazazi wake kwa nadra sana jioni kwa kuwa huwahi kulala. Muda pekee anaokutana nao ni alfajiri anapojiandaa kwenda shule, muda ambao si mzuri kwa mazungumzo.

Kwa kuwa ana hamu ya kwenda Zanzibar, anachukua karatasi na kumuandikia baba yake kumueleza kuhusu safari hiyo, umuhimu wake na mahitaji, ikiwa ni pamoja na fedha anazotakiwa kuchangia. Anaiacha mezani ambako anahisi lazima baba yake akirudi usiku apitie kabla ya kwenda kulala.

Muda pekee wa kujua kama ombi lake limekubaliwa ni alfajiri. Kila anapojiandaa anauliza kama baba yake amemtimizia mahitaji yake hadi hilo linapofanyika.

Maisha ya Praxseda na wazazi wake yanaakisi familia nyingi zinazoishi mijini ambazo ni nadra sana kuwa na muda wa pamoja wa kujadili masuala yao na hata kufuatilia mwenendo wa watoto na kuurekebisha pale inapobidi ili kuendeleza maadili ya familia za Kitanzania.

Matukio mengi yanayotokea hivi sasa-- kuongezeka kwa ukatili ndani ya familia, uhalifu,, kupungua kwa ari ya kusaidiana, watu kushangilia mabaya yanayowapata wenzao, ufisadi, rushwa na uovu mwingine katika jamii-- yanahusishwa na kuyumba kwa malezi katika familia, ambayo ni ngazi ya kwanza ya jamii. “Samaki hakunjwi angali mbichi” na badala yake jamii imejikuta kwenye janga la matukio ya kutisha yasiyoakisi asili ya jamii za Kiafrika. “Mtoto anapaswa kukua akijua majukumu ya baba ni yapi kwa maana ya kichwa na msimamizi mkuu wa familia, mama ni nani kwa maana ya mtu mwenye upendo na anayewakusanya pamoja,” anasema Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa.

“Kutokana na watoto wengi kukosa vitu hivi kutokana na wazazi kubanwa na shughuli za maisha, athari zake zinaonekana ukubwani. Vijana wengi hawana upendo, nidhamu, woga wala hawajali kwa sababu hawakujifunza hayo kwa wazazi wao.”

Ngalalekumtwa, ambaye aliwahi kuwa rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema mtoto anatakiwa kujifunza mambo mema kutoka kwa wazazi wake.

Suala la kukosa faragha na watoto kutokana na kubanwa na shughuli za kimaisha, pia lilizungumzwa na mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa Kiislamu ya Bakwata, Hajaat Shamimu Khan aliyesema pamoja na yote wazazi wanapaswa kutimiza wajibu wao wa malezi.

Alisema malezi yamekuwa changamoto kwenye jamii na yanachangia si tu watoto kuharibika kimaadili, bali pia familia kusambaratika.

“Tunaporudi nyumbani pamoja, tukae nao walau nusu saa kuwasikiliza shida zao na kuwarekebisha walipokosea,” alisema Khan.

“Mtoto aone wewe ni baba na mama yake, hata akifanya jambo jema aseme mlimfundisha nyinyi, akikosa mapenzi ya wazazi na yeye hataona umuhimu wa kuwa karibu na familia yake.”

Alisema wanawake kudai usawa hakuna maana ya kutelekezewa majukumu, bali kusaidiwa na kuongozwa kwa upendo ambao watoto wataurithi kutoka kwao.

“Zamani ilikuwa hakuna shida kumuacha mtoto wa kike na mjomba wake, hivi sasa si rahisi na anaweza kumfanya kitendo kibaya, hivyo ipo haja ya kuwa wamoja,” alisema.

Naye Joliana William, mama wa watoto wawili wenye umri wa miaka miwili na sita, alisema majukumu ya kazi yamemfanya awe mbali na watoto wake.

“Zinaweza kupita siku tano za wiki sijazungumza na watoto wangu,” alisema Joliana.

“Asubuhi wanaandaliwa, nawapeleka shule harakaharaka huku wanasinzia. Nikirudi usiku nakuta wameshalala.”

Joliana alisema inafikia mahali hata wakiumwa hajui hadi aambiwe na dada anayewalea.

“Kama kuna changamoto inayonifanya nisiongeze mtoto ni wasaidizi wa nyumbani. Wana vituko na hawakai (hawadumu), matokeo yake wanangu hawana mtu maalumu wa kumueleza shida zao. Mimi nachelewa kurudi, baba yao ndiyo kabisa, wasichana hawakai,” alisema Joliana.

Matukio ya hivi karibuni yamedhihirisha jinsi jamii inavyozidi kupoteza mwelekeo kutokana na mmomonyoko wa maadili.

Mauaji ya takriban watoto kumi mkoani Njombe yalikuwa ni kiwango cha juu cha ukatili katika miaka ya karibuni.

Bado haijafahamika chanzo cha vifo hivyo, lakini wengi wanadhani imani za kishirikina za watu wanaotaja utajiri wa haraka ndio zilisababisha mauaji hayo.

Wakati mahakama hutoa hukumu kali kwa wahusika wa uovu kama huo ili kuwa fundisho kwa jamii, taarifa zaidi kuhusu wauaji hao hazitolewi na hivyo jamii haijui kinachoendelea kama kutiwa mbaroni kwa wahusika, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa, jambo linaloibua tatizo jingine la kimaadili kwa wafanyakazi wa vyombo vya kusimamia sheria.

Tukio jingine ni la taarifa zisizo sahihi za hali ya afya ya Rais John Magufuli, zilizosababisha nchi kugawanyika, baadhi wakionekana kumuombea mabaya na wengine kumuomba Mungu amsaidie arudi katika afya yake.

Sakata hilo liliisha kwa Rais kujitokeza hadharani wakati akiapisha wateule wake na halijaaibuka tena.

Ili kukabiliana na hali hiyo, baadhi ya taasisi zimeanzisha kambi za vijana kwa ajili ya mafunzo ya kimaadili, uungwana na nyingine kuwakutanisha pamoja kabla ya kurejea nyumbani kuwaepusha kukaa na madada wa kazi, ambao pia wanaonekana chanzo cha kuwayumbisha watoto kimaadili.

Baadhi ya shule pia zimekuwa na ratiba isiyomuweka mwanafunzi muda mrefu shuleni.

“Watoto wangu wanasoma shule ambayo wanatoka saa 11:30 jioni ili kukabiliana na changamoto ya wasichana wa kazi,” anasema Ismail Awadh.

“Muda huo mama yao anakuwa ametoka kazini, hivyo anawapitia na kurudi nao. Ikitokea amechelewa nitafanya hivyo mimi.

“Wakati mtoto wangu wa kike akiwa na miaka mitano, alikuwa ana miguno isiyo ya kawaida, nilipomuuliza akasema amejifunza kwa anko. “Nilipomuuliza anko gani, akasema anayekuja kumtembelea dada yao wa kazi, ambaye hufanya hivyo wakiwa chumbani. Niliudhika na kuanzia hapo sikuwataka wawalee watoto wangu.”

Kwa upande wa Upendo Kimei, mkuu wa shule ya watoto ya Good Hope Day Care, anasema asilimia 75 ya watoto wanaopelekewa ni chini ya miaka miwili na nusu.

Alisema wazazi wengi huwapeleka watoto wao ili kukabiliana na changamoto ya wasaidizi wa kazi wao wakienda kutimiza majukumu yao.

Alisema watoto wenye miaka mitatu hadi sita pamoja na mambo mengine hufundishwa namna ya kujilinda kama kuwaelekeza maeneo ya mwili wanayopaswa kuonyesha na wasiyopaswa.

“Kuna changamoto ya watoto kufanyiwa vitendo viovu, tunawapa elimu itakayowasaidia kujikinga,” alisema.

Alisema muda wa kutoka shule ni saa 10:00 jioni, ila wazazi huwafuata watoto wao saa 11:00 jioni.

“Tunazijua changamoto za wazazi kwa mfano mamalishe, wauza mbogamboga huwa tunawasubiri hadi waje kuwachukua, pia kwa wale watoto wao wenye miaka minne na kuendelea ambao wana watoto wadogo huwa tunawaambia wawaache hapa bure wanaangaliwa pamoja na wenzao,” alisema Upendo Shuleni hapo huwa na amani iliyopitiliza kwa kuwaacha hadi saa 12:00 jioni.

“Mwalimu unalazimika kukaa nao hadi wazazi wao waje, ila wanafunzi wanachoka sana wakikaa hadi muda huo,” alisema Josephine.

Kwa upande wa Upendo Kimei, mkuu wa shule ya watoto ya Good Hope Day Care, alisema asilimia 75 ya watoto wanaopelekewa ni chini ya miaka miwili na nusu.

Alisema wazazi wengi huwapeleka watoto wao ili kukabiliana na changamoto ya wasaidizi wa kazi wao wakienda kutimiza majukumu yao. Alisema watoto wenye miaka mitatu hadi sita pamoja na mambo mengine hufundishwa namna ya kujilinda kama kuwaelekeza maeneo ya mwili wanayopaswa kuonyesha na wasiyopaswa.

“Kuna changamoto ya watoto kufanyiwa vitendo viovu, tunawapa elimu itakayowasaidia kujikinga,” alisema.

Alisema muda wa kutoka shule ni saa 10:00 jioni, ila wazazi huwafuata watoto wao saa 11:00 jioni.

“Tunazijua changamoto za wazazi kwa mfano mamalishe, wauza mbogamboga huwa tunawasubiri hadi waje kuwachukua, pia kwa wale watoto wao wenye miaka minne na kuendelea ambao wana watoto wadogo huwa tunawaambia wawaache hapa bure wanaangaliwa pamoja na wenzao,” alisema Upendo.

Hata hivyo, Beatrice Lawrence Mgumilo mkuu wa kituo cha kulelea watoto cha Ustawi wa Jamii Kurasini, alisema wazazi kutokuwa na muda na watoto kunaathiri kizazi kijacho kimwili na kiakili, wazazi wapo bize na kuwatafutia maisha ya baadaye.

Mzazi hana muda hata wa kuangalia maendeleo ya mtoto, hata mwisho wa juma wanakuwa bize, neno mwanangu nakupenda halipo akiambiwa hivyo na mtu mwingine anamuona anafaa na anaambatana naye.

Alifafanua kuwa hali hiyo inazalisha kizazi kisichokuwa na mwelekeo, ndiyo maana wanaooa na kuoana ndoa zinaporomoka zingali changa, kwa sababu hawana upendo.

Kesi nyingi za ndoa kuvunjika ni vya kawaida, inatokana na misingi watoto hawajajengewa kujua mila na desturi. “Watoto wakati mwingine wanafanyiwa vitendo vya kikatili shuleni au nyumbani, wanataka kuwaambia wazazi wao , wanashindwa kutokana na ubize.”

Chanzo: mwananchi.co.tz