Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikwete ataka huduma afya ya kinywa ziimarishwe

81604c07cb71455c771cb9ed2d5d9740 Kikwete ataka huduma afya ya kinywa ziimarishwe

Sun, 25 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Mrisho Kikwete, amesema bado kuna mahitaji makubwa ya kuimarisha huduma ya afya ya kinywa na meno mkoani Pwani.

Aliyasema hayo Msoga wilayani Bagamoyo wakati wa utoaji elimu na uchunguzi wa matibabu ya afya ya kinywa na meno kwa wananchi wa Kijiji cha Msoga.

Alisema kuwa kuna haja ya halmashauri za mkoa wa Pwani kuendelea kutafuta vifaa tiba ikiwemo “Dental X-ray” kwa ajili ya hospitali.

“X-ray hiyo ipo kwenye halmashauri moja tu katika Mkoa wa Pwani katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia pekee huku halmashauri nane zikiwa hazina kifaa hiki,” alisema Kikwete

. Alisema kupatikana kwa vifaa tiba na wataalamu ni jambo linalowezekana na hivyo, akazitaka halmashauri kujipanga kutatua changamoto hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema huduma za afya ya kinywa na meno zinatolewa katika halmashauri zote tisa za mkoa huo.

Kunenge alisema mkoa una vituo 39 vinavyotoa huduma hizo na kwamba kama mkoa, wanaendelea na juhudi za kuhakisha hospitali zote za halmshauri zinakuwa na vifaa tiba vya kutosha ikiwa ni pamoja na wataalamu na upatikanaji wa huduma ya Dental X-ray aktika hospitali.

Rais wa Chama cha Madaktari wa Kinywa na Meno, Dk Deogratus Kilasara, alisema kuwa mkoa huo umefanya vizuri katika utoaji wa huduma ya afya ya kinywa na meno kwa kuwa huduma hiyo inapatikana katika vituo 39 kati ya vituo 298 vya serikali.

Dk Kilasara alisema huduma hiyo mkoani Pwani zinapatika kwa asilimia 13 ukulinganisha na huduma nyingine za afya na ipo juu ukilinganisha na hali ya kitaifa ambayo hadi sasa ni asilimia saba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz