Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigamboni wanavyopambana kujenga vituo vya afya, hospitali

48963 Pic+kigamboni

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hadi mwaka 2016 Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni haikuwa na hospitali ya wilaya, badala yake kituo cha afya cha Vijibweni kilipandishwa hadhi na kutumika kama hospitali ya wilaya kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo ya jirani.

Desemba 2017, halmashauri ilipokea Sh400 milioni kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi ikiwa ni mpango wa maboresho ya vituo vya afya na kuanza ujenzi Februari 2018 kwa kuwatumia mafundi wajenzi wadogo.

Mfumo huu wa kuwatumia mafundi badala ya wakandarasi wakubwa kama ilivyozoeleka umeonesha mafanikio kwa kuwa majengo mengi yamejengwa na kukamilika kwa gharama ndogo.

Katika kituo cha afya Kimbiji majengo yaliyojengwa na kukamilika ni wodi ya mama na mtoto, maabara, jengo la upasuaji, pamoja na jengo la kuhifadhia maiti.

Majengo haya yamekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa kata za Kimbiji, Pembamnazi, Kisarawe II na wale wanaotoka wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwana ambao wako jirani na kituo hicho.

Hatua ya pili ni ufungaji wa vifaa na katika baadhi ya maeneo vimeshakamilika na kuanza kutoa huduma kama maabara na wodi ya kinamama.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigamboni, Charles Mkombachepa anasema hadi Aprili 2019 vifaa vyote vyenye thamani ya Sh300 milioni vitakuwa vimeshafungwa na kuanza kufanya kazi.

Dk Mkombachepa anasema mara baada ya kuanza upanuzi wa kituo hicho cha Kimbiji, watumishi 32 wa afya walipelekwa kuongeza ufanisi wa huduma.

Julai 2018; halmashauri ilipokea tena Sh400 milioni kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha Afya cha Kigamboni ambacho kabla ya hapo kilikuwa na changamoto ya kuwa na wagonjwa wengi zaidi.

Dk Mkombachepa anasema pamoja na mambo mengine wagonjwa wengi kwenda kutibiwa Kigamboni kunachangiwa na upatikanaji wa huduma bora katika kituo husika. Kauli hiyo inaungwa mkono na diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa akisema kwa kipindi kirefu kituo hicho kilikuwa na sifa ya huduma bora, hivyo anampongeza Rais John Magufuli kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya upanuzi.

Anasema kwa kushirikiana na wananchi na kamati za afya wamesimamia ujenzi ndani ya miezi mitatu na kujenga majengo manne ambayo yapo katika hatua ya upakaji rangi kisha kufunga vifaa.

Hospitali ya wilaya

Mpango wa Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kila wilaya inakuwa na hospitali ya wilaya.

Kigamboni imepokea Sh1.5 bilioni kwa ajili ujenzi huo ambao umeshaanza eneo la Gezaulole, Kata ya Somangila karibu na yanapojengwa makao makuu ya Wilaya na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Ujenzi wa hospitali hii pia unatumia mfumo wa kununua vifaa na kuwakabidhi mafundi kwa ajili ya ujenzi (force account). Tayari majengo saba yameanza kujengwa. Majengo hayo ni utawala, maabara, stoo ya dawa, jengo la X-ray na la kufulia nguo.

Ludigija anasema hadi kukamilika kwa ujenzi huo, Sh7 bilioni zinatarajiwa kutumika katika eneo lenye ukubwa wa hekari 38.

Msimamizi wa mradi huo, Mkuu wa Idara ya Ujenzi Pius Mutechura anasema kiwango hicho kinaweza kupungua kutokana na ushiriki wa wananchi na wadau wanaochangia kokoto, kifusi na mawe. Dk Mkombachepa anasema ujenzi wa hospitali hiyo una manufaa makubwa kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo ya jirani.

Mwandishi wa makala haya ni ofisa habari na mawasiliano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni anapatikana kwa 0713538141 au baruapepe [email protected]



Chanzo: mwananchi.co.tz