Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ametangaza vipaumbele vinne vitakavyokuwa msingi wa juhudi za kutokomeza ugonjwa wa Malaria Afrika ifikapo mwaka 2030.
Kenyatta ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Marais wa Afrika wanaopambana na Malaria (African Leaders Malaria Alliance (ALMA), alieleza hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.
Alisema pamoja na mafanikio makubwa katika vita dhidi ya ugonjwa huo kwa miaka 10 iliyopita, ni muhimu kutafuta na kupata rasilimali zaidi zitakazosaidia kutokomeza ugonjwa huo.
Alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni matumizi ya dijitali na takwimu za mapambano ya Makaria, ushirikiano na mashirika ya kikanda ndani ya Afrika na makundi ya ushauri ya vijana.
Rais Kenytta alisema vipaumbele hivyo vitaleta mapinduzi makubwa, vitatafuta suluhu dhidi ya changamoto za mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo.
Alisema changamoto hizo zinajumuisha ushiriki hafifu wa wanawake, watoto na vijana, uhaba wa fedha toka sekta za ndani, za umma na binafsi pamoja na tishio la kudumaa kwa michango ya wahisani.
Pia Soma
- Chadema waanza mchakato kuwatoa gerezani Halima Mdee, Matiko na Bulaya
- VIDEO: CCM wakamilisha kumlipia Mashinji faini ya Sh30 milioni
- TLP kumteua Magufuli kuwa mgombea wao wa urais uchaguzi mkuu 2020
Kamishina wa Masuala ya Jamii wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Amira El-Fadil, alisema vipaumbele hivyo vimeungwa mkono na Umoja wa Afrika.
Mtendaji Mkuu wa ushirikiano wa kutokomeza Malaria, Dk Abdourahmane Diallo alisema vipaumbele hivyo vikiongozwa na ubunifu na ushirikishwaji wa wadau wote ndio njia sahihi ya kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo.