Sukari ni kiungo kinachotumiwa katika mlo wa kila siku, hasa kwenye vimiminika tofauti. Kwa walio wengi hutegemea sukari kutengeneza kifungua kinywa, chai.
Kwa watoto wadogo sukari ndio kiungo muhimu zaidi kwao kwa kuwa huwekwa kwenye chakula chao, uji.
Bidhaa ikiendelea kuadimika nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema uhaba wa sukari kwenye maeneo tofauti nchini, ni fursa kiafya.
Kwa siku mbili mfululizo kumekuwa na mjadala mkali mtandaoni baada ya Prof. Janabi kupitia ukurasa rasmi wa MNH Instagram kutoa kauli hiyo iliyoambana na picha yake, akitamka:
"Uhaba wa sukari ni fursa ya kubadili mtindo wa maisha, ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza."
Mjadala umevutia wengi kutokana na jina la aliyetoa kauli hiyo, Prof. Janabi, ambaye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari amekuwa na mvuto kwao, akihimiza jamii kutunza afya kwa kula mlo wenye lishe bora.
"Tunasafisha (dialysis) wagonjwa 120 hadi 130 kila siku ya Mungu Muhimbili. Wagonjwa wanaanza kufika hapa saa tisa usiku. Kisukari, shinikizo la damu," anataja magonjwa hayo.
Baadhi ya Watanzania walioufuata ukurasa huo na ambao si wafuasi, walitoa maoni yao kadhaa, huku Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, akiupenda ujumbe huo.
'Usiga' katika ukurasa wake anasema: “Hii sasa 'kiki' daktari, na mwingine akijibu “Ukiwa na akili ndogo hujawahi mwelewa jamaa.”
'Dk. Fransine' alisema: “Katika afya ni sawa, lakini katika siasa haimaanishi vizuri,” huku 'Alexmoshi59’ akisema: "Ninaomba kwenye sukari pawekwe onyo kama kwenye paketi ya sigara. Pia wasiotumia sukari wapunguziwe gharama za bima."
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameunga mkono hoja hiyo ya Prof. Janabi, kuhusu jamii kuepukana na matumizi ya sukari, hasa kipindi hiki cha kuadimika kwa bidhaa hiyo.
"Profesa Janabi oyeeee… kwa lugha nyepesi ukimsikiliza Prof. Janabi anasema, mganga mkubwa sana wa masuala ya afya ya binadamu, ulaji wa sukari uliopindukia una madhara kwa afya. Kwa hiyo, wakati huu sukari imeadimika kidogo, achana nayo," amesema Chalamila.