Wakati Tanzania ikiendelea na utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19, wananchi wametakiwa kuendelea kutumia tiba za asili ikiwemo kujifukiza kwa nyungu kukabiliana namaambukizi ya ugonjwa huo.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Edward Mbanga amewasilisha ombi hilo Ijumaa Agosti 20, alipozungumza na wanahabari kuhusu maazimisho ya siku ya tiba asili ya Mwafrika yatakayofanyika Agosti 28-31,2021 Jijini Dodoma.
Mbanga amesema si jadi kwa Mwafrika kudharau tiba asili kwa kulazimisha kuiga tamaduni za kigeni moja kwa moja japo yapo mambo mazuri ndani yake.
Amesema wataalamu wa tiba asili bado wanaumiza vichwa kutafuta dawa ya Uviko-19 kama ilivyo kwa wale wa tiba za kisayansi ambao nao wanaumiza vichwa.
"Hata hivyo mtu anayedharau tiba asili na kuhusudu dawa za nje moja kwa moja huyo ni mtumwa wa fikra, sina maana dawa za nje hazifai lakini ukweli ni kuwa hata huko wanatumia na tiba asili," amesema Mbanga.
Mbanga amesisitiza uzuri wa tiba asili isipokuwa akapinga suala la ramli chonganishi ambazo zinapaswa kupigwa vita kwa kuwa zinaumiza na kusababisha uvunjifu wa amani.
Amewasihi wananchi kwenye swala zima la utunzaji wa mazingira kwamba ni jambo la muhimu kwani bila kufanya hivyo miti yote itakwisha na hakutakuwa na dawa za asili tena nchini Tanzania na Bara la Afrika.