Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katazo la Wagonjwa wenye Bima ya Afya kuchukua dawa nje ya hospitali lazua mjadala

Waziri Ummy Mwalimu . Katazo la Wagonjwa wenye Bima ya Afya kuchukua dawa nje ya hospitali lazua mjadala

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Baada ya Serikali kuzuia wagonjwa wenye bima ya afya wanaoenda kuchukua dawa au vifaatiba nje ya hospitali, wadau wamesema hatua hiyo inakiuka haki za wanachama na kuwaongezea maumivu wagonjwa.

Katazo hilo la kutumia fomu namba 2C lilitolewa Julai mosi na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa ziarani mkoani Arusha likizizuia kuwaruhusu wagonjwa kwenda kuchukua dawa au vifaatiba visivyopatikana hospitalini.

Utaratibu huo, waziri alisema umekuwa ukiutia hasara Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwani matumizi yake yamekuwa na udanganyifu. Hata hivyo, kutokana na nguvu iliyonayo, wadau wanasema Serikali ingeweza kubuni mbinu mbadala kudhibiti ubadhilifu huo unaofanywa kupitia fomu hiyo si kuwasitishia wananchi huduma waliyoilipia.

“Kuondolewa kwa fomu hiyo kutawakosesha wananchi mbadala wa kupata dawa nje ya hospitali. Mzungunguko huu ni hatari kwamba wagonjwa wengi wasiokuwa na fedha taslim za kununulia dawa kwenye maduka binafsi, watakufa au madhara yatakuwa makubwa zaidi kwao,” alisema Celestine Simba, msemaji wa wagombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Celestine alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa akikiri kuwapo kwa udanganyifu unaofanywa kupitia fomu hiyo lakini akasisitiza kuwa Serikali inatakiwa kuudhibiti kwa njia nyingine si kusitisha matumizi ya fomu hiyo.

“Hili ni tamko batili kwa kuwa linakwenda kinyume na Sheria ya Bima ya Taifa ya Afya ya mwaka 2013 iliyoanzisha fomu hiyo,” alisema Celestine.

Kutokana na umuhimu wa utaratibu huo, Chadema kimeitaka Serikali kulifuta katazo hilo na itafute suluhisho jingine kudhibiti udanganyifu uliopo.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe alisema kutokana na uhalisia ulipo katika hospitali nyingi za umma, katazo hilo ni chanzo kipya cha mateso kwa wagonjwa.

Alisema uamuzi huo umefanywa wakati ambao MSD haina uwezo wa kuhifadhi au kupokea hata asilimia 20 ya dawa muhimu kwa viwango vinavyotakiwa.

Matumizi ya fomu hiyo, alisema yametokana na maduka ya dawa ya Serikali kutojitosheleza hivyo mgonjwa kupata huduma nje lakini yanasitishwa kabla changamoto ya msingi haijatatuliwa.

“Kwa hali iliyopo sasa na ilivyokuwa nyuma, katazo hili litasababisha maumivu mapya kwa wagonjwa. Wagonjwa walikuwa wanapewa nusu dozi ili na wengine wapate, wengine walikuwa wanatakiwa kurudi siku nyingine. Mfumo wa ununuzi wa dawa haujafanikisha upatikanaji wake kila siku,” alisema.

Dk Mwaibambe alisema dhamira ya Serikali kuweka katazo hilo ni kuongeza mapato ya hospitali zake jambo ambalo halipaswi kufanywa kwa kuwagharimu wagonjwa hivyo akaitaka kutathmini sababu za wagonjwa kuhudumiwa kwenye maduka ya nje ya hospitali.

Rais huyo alidokeza kuwa kabla ya katazo hilo la Serikali, baadhi ya hospitali zilianza kuzuia kutoa fomu hiyo matokeo yake wananchi walipata madhara.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa hatua hiyo utafanikiwa iwapo, Serikali imejipanga na itamudu kutosheleza dawa katika maduka yake vinginevyo itasababisha hatari.

Akitoa katazo hilo, Waziri Ummy alisema Hospitali ya Taifa Muhimbili na zile za kanda zilianza kulitekeleza hilo tangu Juni mosi na hospitali za rufaa za mikoa kuanzia Julai mosi akisisitiza kuwa ni jukumu la watendaji wa hospitali kutafuta zilipo dawa na kuzitoa kwa wagonjwa badala ya kuwapa fomu hizo wakazitafute katika maduka binafsi.

“Dawa zipo hospitalini lakini kwa sababu duka la nje ni la kwangu namwandikia mgonjwa aende akachukue nje,” alisema Waziri Ummy.

Akitahadharisha zaidi, Dk Mwaibambe alisema hakukuwa na sababu ya Serikali kuanza utekelezaji wa hatua hiyo haraka, ilipaswa ifanye tathmini katika baadhi ya hospitali kuona tija yake ndipo iendelee kwa hatua nyingine.

“Huwezi kuongeza mapato ya hospitali kwa kumtesa mgonjwa, wagonjwa wasitolewe sadaka kwa ajili ya kuongeza mapato ya hospitali wao si bidhaa,” alisema daktari huyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Maduka Binafsi ya Dawa, Dk Juma Lukobora alisema utekelezaji wa katazo hilo unawakandamiza wao na kwamba kanuni hutungwa kulinda maslahi ya upande mmoja kwa wananchi kuachwa.

“Sisi hii tunapinga kwa kuwa hatuna tulichokosea. Ni kweli wagonjwa hawataacha kuja lakini kuna vibali tutavikosa ambavyo vinatuwezesha kupata hata mikopo katika taasisi za fedha,” alisema Dk Lukobora.

Katazo hili limetolewa wananchi wakisubiri utekelezaji wa sera ya bima ya afya kwa wote ambao muswada wa sheria yake bado haujajadiliwa bungeni.

Mara ya mwisho ilikuwa Mei 19, Serikali iliposema ipo katika hatua za mwisho za kuukamilisha muswada huo jambo ambalo halikufanyika katika Bunge la bajeti hivi karibuni.

Agosti 28 mwaka jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Serikali ilitenga Sh149 bilioni mwaka 2021/22 ili kuanza kutekeleza mpango huo Sh149 bil-ioni katika mwaka wa fedha 2021/22, lakini hadi sasa bado.

“Itaanza kwa makundi maalum kwa wale ambao hawana uwezo wa kumudu gha-rama za matibabu lakini dhamira ya Serikali ni hatua kwa hatua hatimaye Watanzania wote waweze kufikiwa,” alisema Msigwa.

Mpango huo unapendekeza kila mwananchi alipie Sh60,000 kwa mwaka kupata kadi ya bima itakayomwezesha kutibiwa wakati wowote atakapougua.

Muswada huo utakapopelekwa bungeni, wadau wanasema utapaswa kuzingatia changamoto zilizopo na kuziwekea mkakati wa kuzimaliza ili huduma ziwe bora kwa wananchi.

Chanzo: Mwananchi