Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasi ya ujenzi hospitali 10 yaridhisha

300b130c92496246aa9dc35c2878a9bb Moja ya hospitali ya kisasa visiwani Zzanzibar

Fri, 11 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kasi ya ujenzi wa hospitali 10 za Wilaya ya Unguja na Pemba inaendelea vizuri huku wakandarasi wakiahidi kukamilisha kazi kwa wakati zikiwa na ubora wa hali ya juu, imeelezwa.

Akikagua hospitali hizo ikiwemo moja kubwa ya Mkoa wa Mjini Magharibi inayojengwa eneo la Lumumba, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui alisema amefurahishwa na mwanzo mzuri wa ujenzi wa hospitali hizo ambazo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa na kuwapatia wananchi huduma bora za afya.

Aidha, aliwataka wakandarasi waliopewa kazi ya kujenga hospitali hizo kuzingatia ubora na vigezo vinavyokwenda sambamba na mahitaji ya makundi yote kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 36 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya ili kuona huduma za afya zinaimarishwa na kuwa bora kwa wananchi wake.

‘’Wakandarasi mliokabidhiwa kazi ya ujenzi wa hospitali za wilaya matarajio yetu makubwa ni kuona kwamba majengo yanakuwa na viwango vyenye ubora unaokubalika pamoja na mahitaji yote muhimu ya walemavu,’’ alisema.

Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Fatuma Mrisho aliwataka wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa wakati ambayo lengo lake ni kupunguza changamoto za huduma za afya kwa wananchi.

‘’Tunakabiliwa na changamoto katika sekta ya afya ikiwemo msongamano wa wananchi wengi kwenda kupata huduma za afya katika Hospitali ya Mnazi mmoja. Ujenzi wa hospitali za wilaya ndiyo ufumbuzi wake,’’ alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana aliwataka wakandarasi kuhakikisha miradi hiyo ikiwemo hospitali ya mkoa inayojengwa Lumumba kukamilika kwa wakati katika kipindi cha mwaka mmoja na kuepuka visingizio visivyokuwa na sababu.

‘’Uongozi wa mkoa tunafuatilia kwa karibu sana ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Mkoa ambapo matumaini yetu ni kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma za afya,’’ alisema.

Katika ujenzi wa hospitali za wilaya 10 serikali imetenga Sh bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kisasa ya kubeba wagonjwa katika hospitali hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live