Askofu Mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameongoza hafla ya kubariki na kufungua majengo mapya ya Hospitali Teule ya Makiungu inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki Jimbo la Singida na Serikali.
Hospitali hiyo inajengwa kwa wafadhili wa nje kwa gharama ya Sh.10 Bilioni ambao ujenzi wake ulianza mwezi Mei, 2021.
Pengo alisema kuwa upanuzi wa hospitali hiyo utawezesha kuhudumia wananchi wengi na kuwa hafla hiyo imeunganishwa na Jubilee ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo la Singida na kuwa ni jambo ambalo linaeleza nini kimefanyika katika miaka 50 ya kanisa, huku ndani ya kipindi hicho wakiwa wamepiga hatua kubwa.
Alisema wale wote waliohudumia kwa ngazi zote tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo wanamshukuru Mungu na kanisa kwa huduma walioitoa hadi kuwafikisha katika hatua hiyo na wale watakao kuwa wakihudumia wanatarajia watafanya vizuri zaidi ya miaka 50 iliyopita na wataweza kutoa huduma bora kwa watu wenye mahitaji na wagonjwa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Peter Serukamba, alisema serikali ya mkoa huu itahakikisha inajenga hoja ili Hospitali Teule ya Makiungu iliyopo wilayani Ikungi inapandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa lengo la kupanua wigo wa huduma kwa wagonjwa.
Mhe.Serukamba alitoa ahadi hiyo leo (Agosti 17, 2022) wakati wa hafla ya kubariki na kufungua majengo mapya ya hospitali hiyo inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki Jimbo la Singida na serikali ambapo mgeni rasmi alikuwa Askofu Mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. \ “Napenda Askofu Jimbo la Singida, Edward Mapunda nikuhakikishie kwa uwezo wa Mungu tutajenga hoja ili hii hospitali iweze kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,” alisema Mhe. Serukamba.
Alisema yeye (Mkuu wa Mkoa) kwa kushirikiana na viongozi wengine watajenga hoja hiyo hasa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Kanisa Katoliki Jimbo la Singida katika ujenzi wa hospitali hiyo na hivyo namna pekee ya kulishukru kanisa hilo ni kuipandisha hadhi hospitali hiyo ambayo kimsingi inakidhi sifa zote.
Mhe.Serukamba alilipongeza Kanisa Katoliki kwa jinsi ambavyo limekuwa bega kwa bega katika kusaidia serikali katika sekta ya afya na elimu.
Mkuu wa Mkoa aliwapongeza wafadhili wa nje kupitia Padri Alessandro Nava na Dk. Manuela Buzzi na Shirika la Mapadre Wakonsolata waliosaidia ujenzi wa hospitali hiyo ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika Kanisa Katoliki Jimbo la Singida.
Mhe.Serukamba pia alisisitiza suala la upandaji miti katika wilaya zote za mkoa huu na kutaka wananchi waige mfano wa mzuri wa Kanisa Katoliki ambalo maeneo yake yote wanatunza mazingira vizuri kwa kupanda miti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro, alisema tangu wilaya hii ilipoanzishwa mwaka 2012 serikali imekuwa na ushirikiano mzuri na Kanisa Katoliki Jimbo la Singida katika sekta ya afya, elimu na huduma za jamii.
Alisema serikali ya wilaya ya Ikungi itaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki kwani ujenzi wa miundombinu inayoendelea kujengwa Makiungu na Wilaya nzima kwa ujumla itaibadilisha wilaya hii hivyo wananchi wawe tayari kupokea wageni.
Aidha, Muro alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi Agosti 23, mwaka huu kujitokeza kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ili serikali iweze kupata idadi kamili ya wananchi kwa ajili kupanga mipango maendeleo.
Mkuu wa Wilaya alisema wananchi watoe ushirikiano kwa makarani watakaopita kwenye majumba kwa kujitokeza kuhesabiwa ili wilaya ya Ikungi iwe miongoni mwa wilaya zitakazofanya vizuri katika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Kwa upande wake Mbunge Jimbo la Singida Mashariki, Mtaturu alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na nje ya wilaya kwani itakuwa ikitoa huduma kwa bei nafuu sana ukilinganisha na hospitali nyingine.
Mtaturu alisema suala la kuipandisha hadhi hospitali hiyo alishaanza kulifanyia kazi ambapo alishawahi kuwasiliana na aliyekuwa Waziri wa Afya, Dorothy Gwajima. “Nikienda Bungeni hii itakuwa hoja yangu kwa serikali kutaka hospitali hii iweze kupandishwa hadhi ili kuweka msisitizo kwa serikali kwa kuwa waziri alishawahi kutoa ahadi,” alisema.
Naye Askofu Jimbo la Singida, Edward Mapunda, alisema Waziri wa Afya aliwahi kutembelea Hospitali Teule ya Makiungu na kuahidi kuipandisha hadhi iwapo tu itaboteshwa na kuwekewa vifaa tiba vya kisasa kazi maagizo ambayo tayari yameshafanyika.
Awali Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Makiungu Dk.Emmanuel Chidodolo, alisema hospitali hiyo ilifanywa kuwa hospitali teule mwaka 2008 na Julai 2013 ilimegwa kutoka wilaya ya Singida Vijijini.
Alisema hospitali hiyo imekuwa ikipokea ruzuku kutoka serikalini kwa njia ya mfuko wa Pamoja (Basket Fund),dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD) na baadhi ya watumishi wa hospitali wanalipwa mishahara na serikali.
Dk.Chidodolo alisema kama serikali itaipandisha hadhi hospitali hii kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kufanya hivyo itapanua wigo wa huduma zake kwa wagonjwa.
“Endapo hospitali hii itabaki katika ngazi ya wilaya maboresho ya huduma za afya yanayofanyika hapa hayatawanufaisha baadhi ya wagonjwa hasa wateja wa Bima ya Afya madhalani Bima ya Afya ya Taiga (NHIF) ambapo watalazimika kufuata mbali huduma hizo wakati hapa zinapatikana,” alisema Dk.Chidodolo.