Dar es Salaam. Mkurugenzi wa WCB Naseeb Abdul amechangia Sh20 milioni kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto 10 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), huku wasanii walio ndani na nje ya kampuni na wadau wakichangia Sh60 milioni.
Fedha hizo zimepatikana baada ya kampuni ya WCB kuchangisha kiasi cha Sh80 milioni kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Watoto hao wanatimiza idadi ya watoto 90 watakaofanyiwa upasuaji kufikia Desemba na kuvuka idadi ya ahadi aliyoiweka Makonda ya watoto 60 waliotoka katika familia duni kupatiwa matibabu hayo kuanzia Juni 24 hadi Desemba, mwaka huu.
Akizungumza baada ya kutembelea wodi za watoto na vyumba vya upasuaji leo Jumanne Novemba 5, 2019, Diamond amesema alipanga kuwasaidia watoto 10 na tayari ameshalipa Sh10 milioni kama kianzio kwa watoto watano na wiki ijayo atatoa kwa wengine watano.
“Nimepita katika wodi mbalimbali kwa kweli nimeumia sana, watoto wanaumwa na wazazi wao wana hali duni ni ngumu kumudu gharama hizi za matibabu, kupitia kipindi cha Block 49 Wasafi FM, tumeweza kuzungumza na Mheshimiwa Paul Makonda na akaeleza hali halisi mimi nilichanga, wasanii wangu pia wakachanga, kupita kipindi tukapata michango mingi kutoka kwa wasanii wa ndani na Watanzania wengine waliopo nje,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema tangu atoe ahadi yake, leo ni mara ya tano anafika JKCI na tayari ameshatimiza kwa watoto 40 na wengine 10 watafanyiwa upasuaji mapema wiki hii na ijayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi amesema taasisi hiyo ina watoto 512 wanaohitaji upasuaji kwa sasa na wengi wao wapo nyumbani.
“Wanaumwa na wanahitaji msaada wa haraka, hatuwezi kuwaweka hapa wote hatuna nafasi. Kwa sasa tunao 27 ambao wanaendelea kupokea huduma za upasuaji, tatizo ni kubwa kwani kwa kila watoto 100 mmoa anazaliwa na tatizo la moyo na kwa takwimu za mwaka 2018 walizaliwa watoto milioni 2 hivyo kufanya jumla ya watoto 13,000 kuhitaji huduma za upasuaji,” amesema Profesa Janabi.