Dar es Salaam. Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imeagiza wananchi kutii kampeni ya usafi wa mazingira itakayofanyika kesho Jumamosi Juni 8, 2019 kwa lengo la kuangamiza magonjwa ya kipindupindu na homa ya dengue.
Kampeni hiyo inafanyika ikiwa ni siku nne tangu kutolewa kwa takwimu zilizoeleza watu 3,495 waligundulika na ugonjwa wa homa ya dengue na kati yao 3,333 na vifo vitatu ni kutoka katika jiji la Dar es Salaam, huku kipindupindu kikiua watu watatu na wengine 55 kulazwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Juni 7, 2019 Mganga Mkuu wa Mkoa Dk Yudas Ndungile amesema wakuu wa wilaya za jiji wataongoza shughuli hiyo.
"Jumamosi hii Juni 8 tunaanza kampeni ya usafi wa mazingira kuondoa magonjwa ya kipindupindu na homa ya dengue jijini Dar es Salaam, inawezekana kila Mwananchi akishiriki kesho wananchi wajitokeze kwa wingi kufanya zoezi hii," amesema Dk Ndungile.
Amesema shughuli hiyo itashirikisha wananchi katika maeneo husika lakini pia Mwananchi mmojammoja kufanya usafi katika kaya zinazomzunguka.
"Eneo la Kigamboni Mkuu wa mkoa (Paul Makonda) ataongoza katika soko la feri Kigamboni, Ilala waakuwa Jangwani na eneo la Mchikichini, Temeke watakuwa Azimio hivyohivyo Kinondoni na Ubungo nawasihi wananchi wenyewe katika maeneo yao yanayowazunguka wafanye usafi," amesema Dk Ndungile.
Pia Soma
- VIDEO:Mbunge CCM adai TRA chanzo wafanyabishara kukwepa kodi
- MAUAJI MWANAFUNZI SCOLASTICA: Baba mzazi wa mwanafunzi aliyeuawa Scolastica afunguka
- Takukuru yabaini mbinu mpya ya uibaji madini