Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati yataka sheria kuwekeza kwenye kinga

Bunge Pic Data Kamati yataka sheria kuwekeza kwenye kinga

Sat, 12 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bunge limeshauri iundwe sheria itakayosaidia kuwekeza kwenye kinga na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza itakayobainisha kodi ya nyongeza ya bidhaa hatarishi kama vile tumbaku, pombe, vyakula vyenye sukari na chumvi nyingi.

Ushauri huo umo kwenye taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi ya shughuli zilizotekelezwa kwa kipindi cha Januari, 2021 hadi Januari 2022 iliyowasilishwa bungeni na kupitishwa na bunge juzi.

Kupitia taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati, Fatma Hassan Toufiq, wabunge wameshauri iundwe sheria kusaidia wananchi na serikali kuwekeza zaidi kwenye kinga huku ikisisitizwa kwamba sheria itakayoundwa iendane na uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ambapo wananchi watachangia kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

“Aidha, sheria hii ibainishe kodi ya nyongeza ya bidhaa hatarishi kama tumbaku, pombe, vyakula vyenye sukari nyingi na chumvi nyingi. Itatumika kwenye huduma za afya kama sehemu ya kurejesha kwenye jamii iliyoathirika, lakini pia mkakati wa kudhibiti uzalishaji holela wa bidhaa zenye madhara kiafya ili kupunguza uhatarishi,” ilisema taarifa.

Ushauri mwingine ni kwamba serikali itenge ruzuku maalumu ambayo ingeweza kupatikana kama tozo maalumu zitokanazo na biashara ya bidhaa, kama tumbaku, vinywaji vyenye sukari nyingi, pombe, zinazochochea magonjwa sugu yasiyoambukiza na sehemu ya bima za magari kama huduma kwa jamii, kwa kampuni au bidhaa husika.

Kamati ilielezwa kwamba, serikali kwa kutumia vyanzo mbalimbali inatarajiwa kutumia Sh trilioni 12.6 ndani ya miaka mitano ijayo, sawa na wastani wa Sh trilioni 2.3 kila mwaka kupunguza asilimia 15 ya vifo visivyotarajiwa vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Aidha, ilibainika kuwa, zaidi ya asilimia 55.6 ya bajeti ya Wizara ya Afya imeelekezwa katika huduma za saratani, moyo, mishipa ya damu, kisukari, figo, selimundu na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa.

Kamati ilisema magonjwa yasiyoambukiza ni tishio kwa afya za Watanzania wengi kwa zaidi ya asilimia 73.

Aidha, wameishauri Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa (RRH) zisaidie kusogeza huduma za magonjwa sugu yasiyoambukiza karibu zaidi na wananchi na hivyo kupunguza mzigo wa matibabu kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live