Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeshauri serikali kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI katika maeneo ya migodi, vituo vya magari makubwa, maeneo ya mialo ya samaki na maeneo ya starehe kwa kuangalia namna ya bora kutoa elimu kwa wananchi ili kujenga uelewa wa pamoja.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masula ya UKIMWI Stanslaus Nyongo Jijini Dodoma mara baada ya wajumbe kujadili na kuridhia randama ya Bajeti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania –TACAIDS kwa Mwaka wa fedha 2024/2025.
Ameongeza kusema upo umuhimu wa kuweka vituo vya kisasa vya kusambazia mipira (kondomu) ambavyo mhitaji anaweza kuweka tokeni na kupata, utaratibu ambao ni mzuri kabisa na utaondoa utaratibu wa kuchukua mipira hiyo kiholela.
"Kuna baadhi ya sehemu wameanza kutumia mfumo huo wa kisasa wa kusambaza mipira, nasi tuna nafasi ya kuhimiza kuwekwa kwa vifaa hivyo (Kondomu) maeneo mbalimbali ya uwekezaji na maofisini kwa sababu tumepitisha bajeti hii ili muweze kufanya kazi vizuri," amebainisha Nyongo.
Tunahitaji malengo mliyoyakusudia yatekelezwe na yanatimizwe vizuri ili wananchi wapate mazingira mazuri ya kuishi na kuondokana na hali ya maambukizi ya UKIMWI ambayo yanafanya watu waishi katika hali ya wasiwasi.