Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati upotevu bil 1.6/- Hospitali ya Rufaa Tumbi yapewa siku 30

463ebb374873874d585bffb654725a15 Kamati upotevu bil 1.6/- Hospitali ya Rufaa Tumbi yapewa siku 30

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kibaha WAZIRI wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima (pichani)ametoa siku 30 kwa kamati inayofuatilia upotevu wa Sh bilioni 1.6 katika upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi, kutoa tathimini inayoainisha hasara halisi.

Dk Gwajima alibainisha hayo jana wakati akipokea tathimini ya awali ya mradi huo, baada ya maagizo yake aliyoyatoa Desemba 24 mwaka jana, alipotembelea hospitali hiyo na kutoridhishwa na ujenzi huo.

Alikabidhiwa ripoti na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Dk Delphine Magere.

“Namuelekeza Katibu Tawala Mkoa kupitia Kamati yako ya tathimini, mfanye tathimini ya kina ndani ya siku thelathini na kuainisha hasara halisi kwa kurejea vipimo vya jengo zima, kutathimini na kushauri kama jengo hili linafaa kwa matumizi ya umma pamoja na hali ya majengo ya zamani kama yanafaa kukarabatiwa na kutumika tena kwa gharama stahiki,” alisema.

Alitaka kamati kuhakiki uhalali wa uhitaji wa Sh bilioni 29 katika mpango wa upanuzi kwa kurejea michoro ya mpango, kuainisha sababu za wizara kurudia ununuzi wa mkandarasi wa awamu ya pili A na ukidhi wa kisheria katika mchakato huo wa kumnunua mkandarasi mpya.

Vile vile aliagiza mradi huo, usitishwe na madeni yasiendelee kulipwa mpaka atakapopokea tathimini ya kina na kuelekeza vinginevyo.

Katika ziara yake hiyo, Dk Gwajima alitoa maelekezo kwa Katibu Tawala Mkoa kufanya tathmini ya uwapo wa thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi wa upanuzi na uboreshaji wa hospitali hiyo.

Hasara imebainika kwa kuhakikiwa kwa baadhi ya vipimo vya kazi na kuchukua sampuli chache kwa ajili ya vipimo vya kimaabara, jambo lililoashiria kuwapo kwa hasara kubwa zaidi kama ingefanyika tathmini ya kina.

“Ripoti nimeipokea na iko dhahiri kabisa mahitaji ya upanuzi na uboreshaji wa Hospitali ya Tumbi yalikadiriwa kutekelezwa kwa shilingi bilioni 29 baada ya Serikali kuonesha nia ya kusaidia ufadhili wa mradi huo kufuatia mpango wa awali wa uongozi wa mkoa wa mwaka 2007- 2009 uliokuwa na makadirio ya shilingi bilioni tano,” alisema Dk Gwajima.

Alisema mpaka sasa Sh bilioni 9.4 zimekwishatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kati ya Sh bilioni 29 zilizokadiriwa. Alisema Sh bilioni 5.5z imetumika katika utekelezaji chini ya usimamizi wa Shirika la Elimu Kibaha na Katibu Tawala Mkoa na Sh bilioni 3.9 zimehamishiwa Wizara ya Afya.

Hata hivyo, Dk Gwajima alisema taarifa hiyo imebainisha kuwapo kwa mikataba ya wakandarasi wawili, Suma JKT na MUST Construction Bureau kinyume na Sheria Namba 7 ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na marekebisho yake mwaka 2016.

Chanzo: www.habarileo.co.tz