Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kahama yaongoza kuwa na wagonjwa wa TB nchini

Kris Simba Banda la upimaji wa TB

Fri, 25 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imeelezwa kuwa Kiwango cha ugunduzi wa wagonjwa Mkoa wa Shinyanga kimeongezeka kutoka idadi ya wagonjwa 2497 mwaka 2017 mpaka wagonjwa 3157 mwaka 2021 ambapo Manispaa ya Kahama imeongoza kwa kuwa na wagonjwa 1005 ikifuatiwa na Manispaa ya Shinyanga wagonjwa 789, Msalala 451, Kishapu 331, Halmashauri ya Shinyanga 317 na Ushetu 260.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile wakati akitoa Taarifa ya utendaji shughuli za Kifua Kikuu Mkoa wa Shinyanga kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Busungo kata ya Segese halmashauri ya Msalala.

Amesema pia ugunduzi wa watoto wenye Kifua Kikuu Mkoani Shinyanga umeongezeka kutoka asilimia 10.8 kwa mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 22 ya wagonjwa wote kwa mwaka 2021 ambalo ni ongezeko la asilimia 7 zaidi ya lengo la kitaifa na kwamba wameongeza ugunduzi wa wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu na kuanzishiwa matibabu kutoka 2 hadi 11 mwaka 2021 na kupungua kwa vifo vitokanavyo na maambukizi ya Kifua Kikuu kutoka asilimia 16.7 mwaka 2017 hadi 4.7 mwaka 2020.

"Tumefanikiwa kuongeza mashine za kupima sampuli za makohozi kwa kuangalia vinasaba vya bakteria yaani Gene - Xpert kutoka mwaka 2017 hadi 10 mwaka 2021 pamoja na kuongezeka kwa ufanisi wa matibabu (Treatment success) kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu kutoka asilimia 90.5 mwaka 2017 mpaka 96 mwaka 2020", ameeleza Dkt. Ndungile.

"Hali kadhalika tumepunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa 2a Kifua Kikuu kutoka asilimia 4.8 mwaka 202l17 hadi asilimia 2.4 kwa mwaka 2020 na kupunguza watoro wa dawa za Kifua Kikuu kutoka asilimia 4 mwaka 2017 hadi asilimia 0.1 mwaka 2020", amesema.

Amezitaja baadhi ya changamoto katika kutekeleza shughuli za Kifua Kikuu kuwa ni Idadi ndogo ya maabara zinazofanya upimaji wa Kifua Kikuu ambapo zipo kwenye vituo 38 kati ya vituo 262 vya kutolea huduma za afya, utumiaji mdogo wa mashine za upimaji wa Kifua Kikuu kwa kuangalia Vinasaba na ushiriki mdogo wa uibuaji wagonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka vituo binafsi vya kutolea huduma za afya.

Hata hivyo amesema Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (2020-2025) unaendelea kuhakikisha dawa za kutibu Kifua Kikuu zinaendelea kupatikana wakati wote bila malipo yoyote na kuimarisha uwezo wa vituo vya ugunduzi wa Kifua Kikuu kwa kutumia teknolojia mpya ya vipimo kwa kuangalia vinasaba kwa njia ya Gene Expert MTB/RIF na kugatua huduma za Kifua Kikuu sugu.

"Mkoa wa Shinyanga kupitia Wizara unapenda kutoa shukrani nyingi kwa wadau wanaotoa huduma za afua mbalimbali za afya zikiwemo za Kifua Kikuu na UKIMWI ambao ni pamoja na MDH, THPS,FHI 360,SHIDEPHA, RAFIKI,EPIC na vyombo vya habari ambao wamekuwa washiriki wazuri katika kuhakikisha afya za wananchi mkoa wa Shinyanga zinaendelea kuimarika", ameongeza Dkt. Ndungile.

"Kauli Mbiu ya Kifua Kikuu mwaka huu ni 'Okoa Maisha, Wekeza katika kutokomeza Kifua Kikuu nchini' hivyo kila Mtanzania anao wajibu wa kuwekeza katika mapambano ya Kifua Kikuu na kushiriki kikamilifu ili kuwezesha kuutokomeza ugonjwa huu wa TB", amesema Dkt. Ndungile.

Dkt. Ndungile amesema Kifua Kikuu ni ugonjwa sugu wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria (Mycobacterium Tuberculosis - MTB) na kwamba ugonjwa huo husambaa kutoka kwa mtu mmoja mwenye vimelea kwenda kwa mtu mwingine kwa njia ya hewa wakati anapokohoa, anapocheka ama kupiga chafya n.k.

Amezitaja dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu kuwa ni pamoja na homa za mara kwa mara hasa wakati wa jioni,kutokwa jasho jingi kuliko kawaida hata kama ni wakati wa baridi wakati wa usiku, kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu,kupungua uzito na kukohoa wiki mbili au zaidi na kwa watu wanaoishii na Virusi vya UKIMWI ni kikohozi cha wakati wowote.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Chris Simba Liganga TB inatibika hivyo kuwataka watu wenye dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu wafike kwenye vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kuchunguzwa makohozi haraka iwezekanavyo ili kubaini vimelea vya Kifua Kikuu na wale watakaobainika na vimelea kuanzishiwa matibabu mara moja ili kupunguza uwezekano wa kuendelea kuambukiza watu wengine katika jamii.

"Siku ya leo inatukumbusha umuhimu wa kupima Kifua Kikuu kila tuonapo dalili yoyote inayoendana na ugonjwa huu. Pia kupitia wahudumu wa afya wa jamii na waelimishaji rika wanaopita nyumba kwa nyumba naomba muwape ushirikiano ili tuweze kuunganisha hizi nguvu katika kumaliza Kifua Kikuu. Wananchi waendelee kupewa elimu, ushauri na uhamasishaji wa kufika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi wa TB", amesema Liganga.

Aidha Liganga amesema ni marufuku kwa maduka ya dawa za binadamu mtaani kuuza dawa za Kifua Kikuu hivyo kuwataka wananchi kufika katika vituo vya afya ambako dawa za TB zinatolewa bila malipo yoyote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live