Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KUNGURU WEUSI WANACHANGIA ATHARI ZA KIMAZINGIRA, KIAFYA

D845b87de96bb095b7ab71cf945fa7fe KUNGURU WEUSI WANACHANGIA ATHARI ZA KIMAZINGIRA, KIAFYA

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA kipindi kirefu kunguru weusi, wameendelea kuwa kero kubwa katika jamii na viumbe hai vingine. Hawa ni ndege wanaomtegemea binadamu kwa kula mabaki ya vyakula vinavyotupwa ovyo majalalani.

Pia hukamata vifaranga vya kuku, bata na wanyama wengine wadogo wadogo wafugwao. Kunguru mweusi (Indian house crow) asili yao ni kutoka nchi za Kusini – Mashariki mwa Bara la Asia hususani China, Cambodia, Thailand, India na Sri-Lanka.

Hapa Tanzania waliletwa kwa makusudi visiwani Zanzibar na Serikali ya kikoloni mwaka 1890 ikidhaniwa kwamba wanasaidia kusafisha mji.

Wakati huo Mji Mkongwe ulisemekana kuwa na ongezeko kubwa la uchafu. Kati ya mwaka 1950 – 1955 kunguru hao weusi walifika pwani ya Dar es Salaam kwa njia ya majahazi na meli na kusambaa katika mikoa ya Pwani, Lindi, Morogoro, Tanga na Mtwara.

Kilichogundulika baadaye ni kwamba kunguru hawa hawasaidii kumaliza uchafu bali ndio wasambazaji wakubwa wa taka na hivyo Wizara ya Malisili na Utalii kuazimia kuwaangamiza.

Ofisa Wanyamapori wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, Baharia Wasiwasi, anasema moja ya sifa ya kunguru hao ni kuzaliana kwa wingi na kusambaa sehemu nyingi nchini.

Anasema Idara ya Wanyamapori katika Manispaa hiyo imelazimika kutoa elimu endelevu kwa jamii kuhusu namna ya kuwanagamiza.

Wakati wa maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane), Kanda ya Mashariki katikati ya mwaka huu, idara hiyo ilitoa elimu pia kwa wananchi na kuonesha matumizi ya mitego ya kuwanasa kunguru hawa na kuwaangamiza.

Anasema mwaka 2009, idadi ya kunguru weusi iliongezeka maradufu eneo kubwa la Jiji la Dar es Salaam na nje ya mikoa ya ukanda wa Pwani ikiwemo Morogoro na iliyo kando ya Barabara Kuu hadi Dodoma.

Wasiwasi anasema kunguru weusi huharibu bayoanuai pamoja na wadudu wa aina mbalimbali, wanyama wadogo na pia ni wadokozi wa vitu mbalimbali.

Anasema wamekuwa wakisababisha usumbufu mwingi maeneo yenye kupatikana huduma za kijamii hasa vyakula, nyumbani, hospitalini na hotelini.

Anasema kunguru hao kwa sasa wameenda mbali zaidi ya ukanda wa Pwani hadi kufika katika miji ya Bara iliyopo kando kando ya barabara kuu kutokana na kufuata mabaki ya vyakula vinavyotupwa na watu wanaosafiri ama kuishi kwenye mji hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz