Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KCMC yafanya upasuaji wa nyonga kwa mara ya kwanza

Kcmc Data KCMC yafanya upasuaji wa nyonga kwa mara ya kwanza

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wananchi wa Kanda ya Kaskazini ambao walikuwa wakisafiri nchi za nje kufuata huduma za upasuaji wa nyonga, magoti na mabega wameanza kuondokana na adha hiyo baada ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kufanikiwa kufanya upasuaji wa nyonga kwa mara ya kwanza.

Upasuaji huo umefanywa jana Jumanne Februari 15, 2022 ikiwa ni wa kwanza tangu kuanzishwa kwa Hospitali hiyo mwaka 1971.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa Hospitali wa KCMC, Dk Faiton Mandari amesema upasuaji huo utaenda sambamba na maisha halisi ya kitanzania ambapo gharama za ubadilishaji wa nyonga itakuwa ni Sh8.9 milioni na magoti na nyonga utagharimu Sh6.5 milioni.

"Zoezi hili la upasuaji limeanza jana na tunaona kliniki zetu ambazo zimeanza tangu wiki mbili zilizopita ambapo tumeona watu 340 wenye matatizo tofauti yakiwemo ya magoti, nyonga pamoja na mabega na tumepata wagonjwa zaidi ya 20 ambao wapo tayari kwa ajili ya kufanyiwa matibabu na vipimo kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji,"

Dk Mandari amesema uhitaji wa upasuaji huo ni mkubwa kutokana na idadi ya watu wanaoendelea kujitokeza katika Hospitali hiyo kila siku ambapo tayari wagonjwa wawili wa matatizo ya nyonga wameshafanyiwa upasuaji huo jana na afya zao zinaendelea vizuri.

"Huduma hii ni ya kipekee ambapo kwa hapa Tanzania ni hospitali chache ambazo zinatoa huduma hii ya kubadilisha nyonga, magoti na mabega ambayo yameathirika kwa sababu mbalimbali, ila hapa kwetu huduma hii ni ya mara ya kwanza tangu hospitali hii ianze mwaka 1971," amesema Dk Mandari

Advertisement Amesema wengi ambao wana matatizo ya kuathirika kwa nyonga matatizo yao yanatokana na kupata ajali ambayo hupelekea maeneo ya nyonga kuathirika.

"Uwepo wa huduma hii utaleta unafuu mkubwa kwa wagonjwa ambao wameathirika na matatizo haya na  huduma hii  itapatikana kwa urahisi hapa KCMC badala ya  kwenda  nchi za nje na gharama ilikuwa kubwa sana na kuathiri uchumi wa nchi ,"amesema Dk Mandari

Wakizungumza baada ya kufanyiwa upasuaji wa nyonga katika hospitali hiyo, wameishukuru Hospitali hiyo kwa kutoa huduma hiyo na kusema imewapunguzia gharama za kusafiri nje ya nchi pamoja na matibabu.

Musa Suleiman ambaye amefanyiwa upasuaji wa nyonga katika Hospitali hiyo amesema kusogezwa kwa huduma hiyo KCMC itakuwa ni nafuu kutokana na ugumu wa maisha uliopo kwa sasa.

"Kumwambia mtu kwenda nchi za nje kufanyiwa upasuaji huu ambao tumefanyiwa leo ingekuwa ni gharama maradufu ya hizi ambazo tumetoa hapa KCMC kwa kweli hii ni neema kubwa kwa sisi wananchi ambao ni wa hali za chini,"

"Nawashukuru Madaktari wa hapa KCMC kwa kufanikisha kunifanyia upasuaji huu namshukuru Mungu kwasababu nimetoka salama na naendelea vizuri na mazoezi nimeshaanza ," amesema Mussa

Laiki laizer ambaye ni ndugu aliyafanyiwa upasuaji kutoka Ngorongoro amesema ndugu yake anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa nyonga kwani alikuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa muda mrefu.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz