HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), imeanza kutoa huduma ya upasuaji wa kibingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.
Matibabu hayo ya kibingwa KCMC inafanya kwa ushirikiano na Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI).
Mkurugenzi mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface amesema lengo la kuanzisha matibabu ya kibingwa KCMC ni kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda Moi na nchi za nje.
Amesema wamekuwa wakipokea rufaa nyingi kutoka Kanda ya Kaskazini na ushirikiano huo utasaidia kumaliza changamoto ya watu kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kibingwa.
Kwa upande wa Daktari bingwa wa upasuaji wa mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu, KCMC, Honest Massawe amesema hospitali hiyo ina uhitaji mkubwa wa wataalamu waliobobea wa magonjwa hayo kwa kuwa wagonjwa ni wengi wanaohitaji huduma hiyo.