Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Juhudi zaidi zinahitajika mapambano dhidi ya udumavu

5f39fda675544579d5492e370dd5826e.png Juhudi zaidi zinahitajika mapambano dhidi ya udumavu

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UKUAJI wa sekta ya kilimo una umuhimu mkubwa katika kuzalisha chakula cha kutosha ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula na lishe kwa wananchi wakati wote.

Sekta ya kilimo inachangia takribani asilimia 29.1 ya pato la Taifa, asilimia 65.5 ya ajira, asilimia 65 ya malighafi inayotumika katika sekta ya viwanda na asilimia 30 ya pato la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula katika Wizara ya Kilimo, Dk Honest Kessy, anasema serikali imefanya juhudi kubwa ili kuhakikisha sekta ya kilimo inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la udumavu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Dk Tumaini Mikindo, udumavu ni kipimo kizuri cha hali ya utapiamlo kulinganisha na aina nyingine za utapiamlo.

Anafafanua kwamba udumavu ni hali ya akili na mwili wa mtoto kutokua kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na lishe duni na mara nyingi hutokea katika kipindi cha siku 1,000 zinazohesabiwa tangu mimba kutungwa hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili.

Ukuaji wa mtoto mwenye udumavu mara nyingi huwa nyuma kulinganisha na asiye na udumavu na pia ni rahisi kukumbwa na magonjwa licha ya kuwa nyuma kwenye masomo pia.

Dk Kessy anabainisha haya kwa washiriki wa mkutano unaopitia andiko la mpango kazi wa kutekeleza kazi zinazohusu Masuala ya Lishe katika Sekta ya Kilimo.

Anasema kulingana na taarifa ya matokeo ya mapitio ya nusu mwaka ya Mpango wa Kitaifa wa Lishe (Mid Term Review – MTR) ambayo ilifanyika mwaka 2019; imeonesha uzalishaji wa mazao ya chakula hususani zao la mahindi umekuwa ukiongezeka. Dk Kessy anasema kuongezeka huko ni kutokana na msukumo mkubwa uliowekwa na serikali.

Anasema, hata hivyo, kwamba uzalishaji wa mazao mchanganyiko na ulaji usiofaa katika kukidhi mahitaji ya mwili umeonekana kutofanya vizuri na hivyo kusababisha kuwepo kwa udumavu.

Dk Kessy anasema udumavu umepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 32 mwaka 2018 na kwamba ukondefu pia umepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018 ambayo ni chini ya kiwango cha malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) cha asilimia tano.

Licha ya kupungua huko Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula anabainisha kwamba mikoa inayoongoza kwa kuzalisha zao la mahindi imekuwa na changamoto kubwa ya udumavu.

Mikoa hiyo na kiwango cha asilimia ya udumavu wake kwenye mabano ni Njombe (asilimi 53.6); Rukwa (asilimia 47.9); Iringa (asilimia 47.1); Songwe (asilimia 43.3); Ruvuma (asilimia 41) na mkoa wa Kigoma (asilimia 42.3).

Dk Kessy anaongeza kuwa mtoto akishakuwa na udumavu hakuna tena tiba hata kama atakula baadaye lishe bora lakini atakuwa ameathirika na kwa sababu hiyo kuna haja ya kuunganisha juhudi kwa wadau wengi kuweza kupambana na hali hiyo.

“Niseme kuwa udumavu hauna tiba, mfano udumavu ukimpata mtoto mdogo, hali hiyo inaathiri maisha yake yote pamoja na makuzi na afya ya ubongo wake na mtoto kama huyo hata darasani hawezi kuelewa vizuri masomo yake,” anasema Dk Kessy.

Pamoja na haya anasema, Wizara ya Kilimo ni miongoni mwa Wizara zinatotekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (National Multi- sectoral Nutrition Action Plan) ulioanza kutekelezwa mwaka 2016 na unataraji kumalizika mwaka 2021.

Dk Kessy anasema Wizara ya Kilimo pia inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili ( ASDP II) ambapo mikakati yote imetambua umuhimu wa kilimo katika kuboresha lishe.

Anasema mpango kazi wa miaka mitano wa kutekeleza kazi zinazohusu lishe katika sekta ya kilimo, hasa masuala ya lishe ni miongoni mwa mikakati ya kukabili changamoto ya utapiamlo kwa Watanzania. Dk Kessy anasema licha ya juhudi hizo bado kuna haja kwa wadau wote kushirikiana na serikali kuendelea kupunguza kiwango cha utapiamlo na udumavu nchini.

“Juhudi zinapaswa kulenga katika kuongeza uelewa, kuelimisha watu kuhusu tamaduni na kuongeza uelewa namna nzuri ya kubadili maisha ya watu kila siku kuhusu ulaji wa vyakula vya makundi yote,” anasema Dk Kessy.

Katika kuunga mkono juhudi hizo ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii elimu lishe, Kampuni ya Sanavita ya mkoani Morogoro inatekeleza mpango wa utoaji wa elimu ya lishe kwa wadau wa afya, elimu, ustawi wa jamii na viongozi wa dini.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Jolenta Joseph, anasema makundi ya wadau kama hao wakipewa elimu ya lishe watakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha lishe kwenye jamii na hasa kwenye shule za msingi na sekondari.

Jolenta ambaye ni mtaalamu wa masuala ya lishe licha ya mkakati huo wa utoaji elimu ya lishe, anasema upungufu wa damu unaosababishwa na upungufu wa madini ya chuma ni mkubwa kwa wajawazito, wanaonyonyesha na kwa watoto waliofikia umri wa rika balehe.

Mkurugenzi huyo anasema kwa kutambua tatizo hilo kampuni ya Sanavita inajishughulisha na uzalishaji wa mazao ya kibaolojia yenye virutubisho vingi. Mazao hayo ya kibaolojia ni pamoja na viazi lishe wenye vitamin A kwa wingi, mahindi lishe na maharage lishe ambayo yana madini ya chuma pamoja na zinki.

Jolenta, anasema lengo kubwa la kutolewa kwa elimu hiyo kwa wadau hao ni namna ya kuongeza uelewa kwenye jamii kuhusu mazao hayo na nafasi yake katika kuboresha lishe kwa binadamu.

Anasema kuna tatizo kubwa la utapiamlo hasa njaa iliyofichika na upungufu wa damu unaosababishwa na upungufu wa madini ya chuma ni asilimia 44.7. Jolenta, anasema upungufu huo wa damu ambao unasababisha vifo vingi kwa wajawazito na wanaonyonyesha lakini pia kwa watoto wanaofikia umri wa rika balehe.

“Lengo letu kubwa la uzalishaji wa mazao yaliyorutubishwa kibaolojia na yenye viritubisho vingi ni mpango mkakati na endelevu unaolenga kupunguza tatizo la utapiamlo nchini,” anasema Jolenta.

Mkurugenzi huyo, anasema katika utoaji wa elimu ya lishe tayari wamewafikia wanajamii 20,000 wakati wakulima 2,000 wamejitokeza kuzalisha mazao ya viazi lishe, mahindi lishe na maharange liche na hivyo kuwa na soko la uhakika. Jolenta anasema Sanavita itaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya lishe na ulaji unaaofaa kwa kuwafikia watu takribani 40,000 kwa mwaka 2021.

Katika kuendeleza mkakati hiyo, anaziomba mamlaka husika na watoa uamuzi kuzitaka shule zote ambazo zinatoa chakula kwa wanafunzi watumie bidhaa zenye lishe bora. Bidhaa hizo ni pamoja na mahindi lishe, maharage lishe na viazi lishe ili kupunguza matatizo ya utapiamlo kwa wanafunzi hususani waliopo shuleni.

Naye Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Muungano wa Kimataifa wa Kuimarisha Lishe (GAIN) hapa nchini, Gaston Amos, anasema kwa kutambua changamoto hiyo shirika hilo limekuwa likifadhili mashirika madogo madogo yanayojihusisha na utoaji wa lishe sehemu za shule, sokoni na magerezani na Sanavita ni miongoni mwa wanufaika na ufadhili huo nchini.

“Hadi sasa tumetoa mikopo ya takribani dola 300,000 kwa mashirika matano ya hapa nchini yanayojishughulisha na lishe na tunataa viributisho lishe kwenye mahindi kwa maana ya sembe, mafuta ya kula na unga wa ngano,” anasema Amos.

Nao baadhi ya wanufaika wa elimu ya lishe kwa nyakati tofauti walieleza kuwa elimu waliyoipata imewawezesha kuwa na ufahamu mkubwa kuhusiana na masuala ya lishe hasa kwa wanafunzi shuleni kwa kuwa shule nyingi zinakuwa na utaratibu wa utoaji wa uji kwa wanafunzi wa madarasa ya awali pasipo kuzingatia umuhimu wa lishe bora.

Mratibu wa mradi wa Lishe Endelevu Mkoa wa Morogoro, Mariam Mwita, anasema suala la lishe kwa sasa ni mtambuka na hivyo anaishauri jamii kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Serikali ili kuhakikisha wanajenga vizazi vyenye watoto wenye afya na lishe bora.

Chanzo: habarileo.co.tz