Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jitihada zaanza kukabiliana na kirusi kipya cha Corona

Kirusipic Data Jitihada zaanza kukabiliana na kirusi kipya cha Corona

Tue, 30 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati waliochanjwa kinga ya virusi vya Uviko-19 wakihofu huenda wakalazimika kuchanja tena kukabili kirusi kipya cha Uviko-19, Wizara ya Afya imesema imeshaanza kuchukua hatua kukabiliana nacho.

Kirusi hicho kinachoitwa Omicron, kinaelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kukwepa kinga iliyojengeka baada ya kuchanja.

Watalaamu wa afya nchini wamesema hilo linatokana na kirusi hicho kujibadilisha mara 30, kwa kuvaa protini tofauti na hivyo kuja na nguvu kubwa ikilinganishwa na virusi vya awali.

Tayari kuna taarifa za kuambukizwa watu zaidi ya 70 katika jimbo la Gauteng, Afrika Kusini, wanne Botswana, mmoja Hong Kong, matukio hayo yakihusishwa na watu kusafiri kutokea Afrika Kusini.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale amesema tayari wameshachukua hatua za kukabiliana na kirusi hicho, huku akisisitiza wananchi kujitokeza kupata chanjo.

“Kutokana na hali hii hatuna budi kuendelea kuchukua hatua sahihi za kujikinga dhidi ya ugonjwa huu.Wizara inasisitiza kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuendelea kujitokeza kupata chanjo,” alisema.

Dk Sichwale alisema chanjo zimeonyesha ufanisi mkubwa dhidi ya madhara ya Uviko-19.

Aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari huku nchi ikiendelea kuimarisha uchunguzi wa wasafiri katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu na kufanya ufuatiliaji wa nchi zenye ongezeko la wagonjwa na kuchukua hatua stahiki.

Mapema, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Shadrack Mwaibambe alishauri watu kuchanja chanjo nyingine ya ‘booster dose’ ili kuimarisha zaidi kinga.

“Kirusi hiki kimebadilika mara 30, kina uwezo mkubwa wa kukwepa kinga iliyojengeka baada ya kuchanja, hivyo chanjo ya zaidi yaani kama ulichanja Johnson&Johnson ukachanja tena Pfizer unaongeza kinga zaidi,” alisema.

Dk Mwaibambe alisema wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na Uviko-19.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati alisema kirusi hicho kimetengeneza protini mabadiliko ambayo haijawahi kuonekana kwa kirusi cha Uviko-19 au cha aina nyingine.

“Hiki ni kirusi cha kwanza kilichojibadilisha mara nyingi, protini zaidi ya 30, kingine 32 ukilinganisha na hivi vingine viwili kikiwemo cha delta kilichojibadilisha mara mbili, ambacho hata hivyo kilileta shida Afrika Kusini na India,” alisema.

Dk Osati alisema kutokana na kujibadili huko, inaleta wasiwasi mkubwa kwa wanasayansi kwamba inaweza kuwa ni hatari kuliko vilivyotangulia, kwani huenda kikawa na uwezo hata wa kukwepa kinga za mwili na kudhuru zaidi.

Alisema kirusi hicho kinaweza kugundulika kwa vipimo vya kawaida, lakini bado hakuna taarifa zaidi kukihusu iwapo chanjo zilizopo zinafaa au la.

“Pia hakuna jibu la moja kwa moja kama kinaweza kusababisha ugonjwa mkali, ingawa inaelezwa kinawaathiri pia vijana na kinafika haraka kwenye mapafu kuliko aina ya virusi vilivyopita,” alisema Dk Osati.

Alisema wagonjwa wengi hawajapata homa bali walihisi kuchoka, lakini baadaye walipata nimonia ya Uviko-19 ,hali hiyo inaleta wasiwasi.

“Kinachosababisha hatujui sana, lakini kadri ugonjwa unavyokaa kwa binadamu kwa muda mrefu wale virusi wanajifunza tabia za mwili na kinga za binadamu na huanza kubadilika,” alisema.

Dk Osati alisema mabadiliko hayo yametokana na watu kutojikinga kwa chanjo. “Tunasisitiza watu wafuate afua za chanjo kwa kuvaa barakoa na kinga nyingine kwa mazingira yetu chanjo zinaweza kuzuia kwa kiasi kikubwa na muhimu ni kuendelea kuchanja,” alisema Dk Osati.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Aga Khan, Alex Masao alisema ni mapema sana kuuzungumzia ugonjwa huo na kirusi hicho kwa sababu bado utafiti wa kina unahitajika.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limekitangaza kirusi hicho kipya kuwa chenye kutia wasiwasi na kukiita jina la Omicron, hivyo kukiweka katika kipengele cha aina ya kirusi cha Uviko-19, kinachosumbua zaidi pamoja na kile cha delta.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live