Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Jinsi vidonge vya uzazi wa mpango vilivyotaka kuniua’

296f732be0c097889b51ea825f4f0a56 ‘Jinsi vidonge vya uzazi wa mpango vilivyotaka kuniua’

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

Vanessa Centeno alipobaini kuwa ana damu iliyoganda inayoziba mapafu yake ilikuwa kitu kigumu sana kwake kukikubali. Lakini alipobaini chanzo cha hali hiyo akachanganyikiwa zaidi.

Mwaka 2019, mwanamke huyo aliyekuwa anaishi Boston, kama ilivyo kwa mamilioni ya wanawake wengine duniani alikuwa akitumia dawa za kupanga uzazi.

Lakini tofauti na wanawake wengine, Venessa alianza kudhurika kwa kutumia vidonge kama njia ya mpango wa uzazi, damu ikaanza kuganda iliyobadilisha kabisa maisha yake.

Nilidhani ni mshutuko wa moyo "Nilikuwa ninatembea kwenye ngazi na ghafla pumzi zikaanza kubana hadi nikaanza kushika kijisanduku cha kuweka barua kwa sababu sikuweza kupumua," Vanessa anakumbuka.

"Sijawahi kuhisi kupoteza pumzi namna hiyo na nilikuwa ninajitahidi kwa kila namna niweze kupata hewa safi," anaongeza. Licha ya kukumbwa na hali hiyo, Venessa aliamua kwenda kazini baada ya kuhisi nafuu lakini akatoka mapema ili akamuone daktari.

"Walinipatia dawa ambayo inatakiwa kufungua njia ya kuingiza hewa. Nikaanza kupata nafuu na kuanza kupumua kiasi.

Walinipiga picha na kusema kuwa wameona kitu kama kivuli kwenye mapafu yangu wakahisi kwamba lilikuwa tatizo la uvimbe kwenye mapafu au nimonia," Lakini kilichofuata, kliniki hiyo ikamuarifu Vanessa kwamba haukuwa ugonjwa wa mapafu na kwamba alihitaji kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu zaidi.

Hata hivyo, Vanessa hakuweza kuonana na daktari kwa karibu mwezi mzima, hali yake ikaanza kudorora na kliniki hiyo ikamshauri aanze kutumia bomba la dawa ya kupitisha oksijeni, dawa inayotumika na wagonjwa wa pumu.

"Lakini hali hiyo ikatokea tena…Nilikuwa ninapanda ngazi na kushuka nikiendelea na kazi zangu za nyumbani kama kawaida lakini ghafla nikaanza tena kupata matatizo ya kupumua na nikaamua kufungua upande mmoja wa nguo ili nipate hewa safi lakini kilichofuata nilijikuta nimeanguka sakafuni.

"Mwili wangu ulikuwa unauma; tumbo langu, kifua changu, mikono yangu, vyote vilikuwa vinauma na hapo nikaanza kufikiria kuwa nimepata mshutuko wa moyo."

Siku hiyo Vanessa anasema hakwenda hospitali badala yake akampigia daktari wake, muuguzi akamuagiza kufika hospitalini haraka iwezekanavyo.

"Siku iliyofuata, nilikwenda kumuona daktari na kumueleza dalili zangu zote na baada ya kunikagua akataka nipigwe picha ya CT Scan, na hapo ndipo nilipoelekezwa kufika katika hospitali kubwa.

"Huko nikawekwa katika vifaa chungu nzima kufuatilia hali yangu, nikaanza kupewa matibabu kwa njia ya mishipa, yaani kila kitu kilitokea haraka sana kiasi cha kuanza kuchaganyikiwa."

"Ikabainika kuwa damu yangu imeganda kifuani na mgando huo umeanza kupasuka pasuka na kuziba mapafu yangu." Vanessa alikuwa hospitali kwa siku mbili ndipo akaruhusiwa kurejea nyumbani lakini akatakiwa kupumzika nyumbani kwa wiki mbili.

Madaktari walisema kuwa sababu kubwa iliyochangia hali hiyo ni kubadilisha njia ya mpango wa uzazi na hicho ndicho kilichoonekana kama kitu kigeni mwilini mwake.

Anasema madaktari walimuarifu kuwa ikiwa angemaliza siku moja zaidi bila kupata tiba kuna uwezekano mkubwa angepoteza maisha kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya.

Tatizo linawapata akina mama wangapi? Ni tatizo la nadra lakini lipo, ndivyo wanavyosema watalaamu.

Kulingana na taasisi ya huduma ya afya ya taifa nchini Uingereza, kuna matukio 5 hadi 12 kati ya wanawake 10,000 ambao hupata tatizo la kuganda damu kwa mwaka kutokana na matumizi ya dawa za uzazi wa mpango.

Duniani, zaidi ya wanawake milioni 150 wanatumia vidonge kama njia ya mpango wa uzazi na ndio njia inayotumika sana Ulaya, Australia na New Zealand.

Pia njia hiyo ni ya pili kwa umaarufu barani Afrika, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini huku barani Asia ikiwa ya tatu. Vidonge kama njia ya mpango wa uzazi kama nyingine yoyote ile ina athari zake zinazofahamika sana ambazo ni pamoja na hisia za mapenzi kubadilika-badilika na ama kuongeza uzito au kukonda.

Kwa upande mwingine miongoni mwa athari zisizofahamika sana za utumiaji wa vidonge kama njia ya upangaji uzazi ni kuganda kwa damu ambako kunaweza kuhatarisha maisha.

Hatari ya wanawake kuanza kuganda damu kunasababishwa na homoni, umri, historia ya familia ya tatizo hilo na mtindo wa maisha kama vile uzito wa mwili na kuvuta sigara. Mfumo dume unatatiza wanawake Zaidi ya mwaka mmoja tyangu atokewe na hali hiyo na kupata tiba, Venessa bado hajaweza kurejea katika hali yake ya kawaida.

"Ghafla, nilijikuta nikiwa na uvimbe wa damu kwenye mishipa ya mapafu na nikalazimika kuanza kutumia dawa kwa miezi sita. Kisha nikalazimika kuwa makini nisianguke au kujikata kwa sababu chochote kile kinaweza kusababisha kuvuja damu kwa ndani.

"Kila wakati nalazimika kujikumbusha kwamba niko sawa na sasa siko katika hatari yoyote tena." "Sijui kwanini ilitokea kwa sababu nimekuwa nikitumia njia za uzazi wa mpango kwa kipindi kirefu," anasema.

Anasema aliwahi pia kutumia ya upandikizaji lakini ikawa inamfanya kuongeze uzito. Vanessa anasema kuishi katika dunia yenye mfumo dume kunafanya wanawake kubeba mzigo mzito ikiwemo kuhakikisha mwanamke unatumia njia angalau moja ya mpango wa uzazi.

Anapendekeza wanaume pia wawe makini katika kupanga uzazi na siyo jukumu hilo kulitupa kwa mwanamke zaidi. Mbali na kutumia kondomu au njia za asili ikiwemo ya kuishia nje, njia nyingine ambayo mwanaume anaweza kupanga uzazi ni inayoitwa vasectomy.

Vasectomy ni upasuaji mdogo ambao humfanya mwanaume asiweze tena kusababisha mimba maishani mwake akishafanyiwa lakini huendelea kufurahia tendo la ndoa kama kawaida.

Makala haya bila kuongezewa uhariri, kwa mara ya kwanza yalichapishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Januari 12, 2021.

Chanzo: habarileo.co.tz