Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi kuchelewa kula usiku kunavyohatarisha maisha yako

8252493c7eee4db130a336640fa7cdaa Jinsi kuchelewa kula usiku kunavyohatarisha maisha yako

Mon, 4 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MTAALAMU wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFCN), Adeline Munuo amesema kuchelewa kula chakula cha usiku kabla ya kulala ni hatari kwa afya.

Aliieleza HabariLEO jana kuwa ili kuwa na afya bora ni muhimu mtu ale angalau saa mbili kabla ya kulala.

Alisema mtu anayekula usiku muda mfupi kabla ya kulala hujiweka katika hatari ya kuongezeka uzito kwa sababu mwili unakuwa katika hali ya mapumziko hivyo hushindwa kumeng’enya chakula ipasavyo.

"Na matokeo yake chakula hubadilishwa kwenda kwenye mafuta na kuhifadhiwa hivyo kuongeza uzito.”

"Pia, usiku ni muda ambao mwili hufanya kazi nyingine ikiwamo kutengeneza seli zilizoharibika hivyo mwili hushindwa kufanya kazi hii endapo utakuwa unashughulikia mmeng’enyo wa chakula hivyo kuuweka katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa kiurahisi," alisema Munuo.

Alisema kutozingatia muda wa kula ni moja ya sababu zinazochangia kutokuwa na afya bora.

"Kuchelewa kula kunaweza kusababisha ulaji wa chakula kingi kuzidi mahitaji ya mwili kwa wakati huo hivyo kupelekea kuongezeka uzito wa mwili. Uzito uliozidi ni kihatarishi cha magonjwa sugu yasiyoambukiza," alisema. Aidha, Munuo alisema ili mtu kuwa na afya bora ni muhimu kula chakula mchanganyiko kutoka makundi tofauti tofauti ya vyakula.

"Kula matunda na mbogamboga kwa wingi kila siku ili kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali. Ongeza ulaji wa vyakula vyenye makapimlo kwa wingi kama nafaka zisizokobolewa, mbogamboga na matunda kwa wingi ili kuwezesha mfumo wa chakula kufanya kazi kwa ufanisi.”

"Pia makapimlo husaidia upatikanaji wa haja kubwa kiurahisi na kupunguza uwezekano wa kuongezeka uzito, kupata maradhi ya saratani, magonjwa ya moyo na kisukari,” alisema.

Kwa mujibu Munuo, mahitaji ya chakula yanategemea umri, jinsia, aina ya kazi mtu anayofanya na hali ya kifiziolojia ya mwili mfano mgonjwa, mjauzito, mzee au mtoto.

Chanzo: www.habarileo.co.tz